Mambo matano yanayomuondoa Benchikha Simba

Usiku wa leo Simba itakuwa uwanjani mjini Unguja kumalizana na Azam kwenye  pambano la fainali ya michuano ya Kombe la Muungano litakalopigwa Uwanja wa New Amaan, huku mabosi wa klabu hiyo wakianza kukuna vichwa kutokana na taarifa kwamba Kocha Mkuu, Abdelhak Benchikha anajiandaa kuondoka klabuni.

Taarifa ambazo Mwanaspoti imehakikishiwa na baadhi ya mabosi wa Simba ni kwamba kocha huyo anajiandaa kuondoka mwishoni mwa msimu huu, huku kukiwa na upepo uliomtibua tofauti na matarajio ya wengi tangu klabu hiyo ilipomtangaza kuwa mrithi wa Mbrazili Roberto Oliveira ‘Robertinho’ aliyefutwa kazi baada ya zile 5-1 ilizopigwa Simba katika Kariakoo Dabi kutoka kwa Yanga.

Hata hivyo imekuwa ikifanywa siri juu ya jambo hilo la Benchikha kuwaambia mabosi kwamba mwisho wa msimu ataondoka klabuni, lakini baadhi ya mabosi wa klabu hiyo wamekiri suala hilo lipo na hapa chini Ukiondoka misimamo mikali aliyonayo kocha huyo katika kile anachokiamini ambacho wakati mwingine kimekuwa kikiwazingua wachezaji na hata mabosi wake, lakini hapa chini Mwanaspoti linakuletea mambo matano yanayomuondoa kocha huyo Mualgeria aliyeajiriwa mwishoni mwa Novemba, mwaka jana.

Inaelezwa mara baada ya kufika Simba, Benchikha alitaka kupatiwa nyumba akitoa masharti ya nyumba anayoitaka na mabosi wa klabu hiyo wakaingia msituni kuisaka nyumba hiyo, lakini katikati ya msako huo jamaa akasitisha mpango huo.

Nyumba ambayo Benchikha aliitaka ilikuwa ya gharama kubwa akitaka kukaa kando mwa Bahari ya Hindi maeneo ya Masaki, na alitaka kuileta familia yake nchini kutoka Ufaransa.

Benchikha aliwazuia mabosi wa Simba wasiendelee na mchakato wa kumtafutia nyumba akiwaaambia atabaki palepale anapokaa sasa, hatua ambayo iliwaacha njiapanda viongozi wake wasijue kipi kimesababisha uamuzi huo.

Baada ya kukiona kikosi cha Simba, Benchikha alihitaji usajili wa hatua mbili – kwanza ule wa dirisha dogo, imeelezwa kuwa katika wachezaji ambao aliwataka hawakupatikana kutokana na gharama kubwa ambayo Simba ilishindwa kumudu kuwanasa na mwishowe kusajili wachezaji ambao hawakuwa kwenye hesabu zake hasa baada ya kutemwa kwa mastraika Jean Baleke na Moses Phiri.

Simba ilisajili wachezaji kadhaa wakiwamo wazawa na kwa wale wa kigeni ambao ndio ilikuwa hesabu za Benchikha aliishia kuletewa Freddy Kouablan na PA Omar Jobe ambao viwango vyao hakukubaliana navyo.

Wakati huu ambao Simba inapiga hesabu za kufanya usajili mkubwa alikutana na viongozi wa klabu hiyo kabla ya kukutana na Yanga akasisitiza juu ya aina ya wachezaji ambao anaamini watamfanya kufikia malengo, lakini hilo likabaki palepale kukwama kwenye bajeti kubwa ambayo ingehitajika.

Na kichapo cha mabao 2-1 ilichopata mbele ya Yanga katika Kariakoo Dabi kikaongeza hasira kwake, kwa kuamini angekuwa na wachezaji aliokuwa anawahitaji huenda angeizuia Yanga iliyoshinda mechi ya duru la kwanza kwa mabao 5-1 na kibaya zaidi ni kwamba yeye ni kocha asiyependa kupoteza mechi kizembe.

Wakati anapewa ajira Msimbazi, klabu ya Simba ilimpa Benchikha malengo ya kufika nusu fainali au hata fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. kocha huyo alikubaliana nalo na kuanza kazi, lakini baada ya kuanza akaona aina ya kikosi alichonacho hakiendani na malengo hayo.

Benchikha ameona aina ya kikosi cha Simba kilichopo sasa kinahitaji nguvu kubwa ya kukijenga kwa ubora ili kiweze kucheza na kuwa kati ya timu nne zitakazocheza nusu fainali au hata fainali ya mashindano ya klabu Afrika akijiridhisha pia na ufinyu wa maboresho ya wachezaji ambao anawataka kuonekana kuwa na ugumu kwa Wekundu hao kuwapata.

Matokeo yake ni kwamba Simba iliishia robo fainali ya michuano hiyo ya Afrika, lakini ikatolewa pia katika 16 bora ya Kombe la Shirikisho (FA) moja ya mataji aliyokuwa na kazi ya kuyarejesha Msimbazi likiwamo la Ligi Kuu Bara ambayo yote yanashikiliwa na Yanga kwa misimu miwili mfululizo.

Wakati Benchikha akiendelea kuielewa Simba nje alikuwa akipambana kuzima tamaa ya ofa nyingi kubwa ambazo anazipokea kutoka kwa klabu kubwa na mataifa makubwa ambayo yanahitaji huduma yake.

Simba ikiwa haijatulia huku nje akawa anakumbana na presha hiyo ya kuhitajika na klabu ambazo anaamini anaweza kuwa na wakati mzuri wa kufanya majukumu yake kuwa rahisi. Hilo nalo limemsukuma kufikia uamuzi huo.

Ndani ya Simba nako kuna ukweli ambao ulikuwa hauwaingii baadhi ya viongozi wa klabu hiyo, kocha huyo aliyetambulishwa Novemba 24,2023 kuwa kocha mpya wa Wekundu hao ameiongoza timu hiyo kucheza mechi 24 za mashindano yote kabla ya fainali ya jana dhidi ya Azam ya Muungano.

Kwenye mechi 24 zimo za Ligi ya Mabingwa Afrika mechi saba – akishinda mbili akitoka sare mbili na kupoteza tatu, na kwenye Ligi Kuu Bara akiiongoza Simba mpaka sasa kucheza mechi 13 ndani yake akishinda nane, sare tatu na kupoteza mbili wakati Kombe la Shirikisho akiiongoza Simba kucheza mechi tatu akishinda mbili na kupoteza moja.

Simba ilikuwa Unguja, Zanzibar ikishiriki mashindano ya Kombe la Muungano na ikiwa ilishinda mechi moja ikisubiri usiku wa jana kucheza fainali dhidi ya Azam rekodi hiyo sambamba na aina ya mpira ambao Wekundu hao wanacheza bado kuna baadhi ya vigogo wanaona kuwa bado kocha huyo hajaibadilisha kwa ukubwa timu yake hatua ambayo iliwafanya kuanza kuwa na mashaka na mwenendo wake.

Related Posts