Same.Watu watatu wa familia moja, katika kitongoji cha Kampimbi, Kijiji cha Ndungu, Wilaya ya Same, Mkoani Kilimanjaro wanadaiwa kumshambulia na kumuua kwa kumkata sehemu za kichwa na begani na kitu kinachodhaniwa kuwa na ncha kali, Mwenyekiti wa kitongoji cha Sinangoa A, Charles Mkuruto na kumsababishia kifo chake.
Mwenyekiti huyo ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la ardhi kata ya Ndungu, aliuawa jana Aprili 26, mwaka huu baada ya ndugu hao kudaiwa kumvamia na kumshambulia na kisha kutokomea kusikojulikana.
Inadaiwa kuwa mauaji hayo yanatokana na uwepo wa mgogoro wa ardhi unaobishaniwa na wanafamilia hao katika Kijiji hicho kwa muda mrefu ambao tayari upo katika Baraza la ardhi la kata.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Mkuu wa Wilaya hiyo, Kasilda Mgeni amesema tukio hilo limetokea jana, Aprili 26 muda wa saa 5:30 asubuhi maeneo ya kitongoji cha Kampimbi kata ya Ndungu na baada ya tukio hilo kufanyika watuhumiwa wa mauaji hayo walitoroka.
DC Mgeni amelaani vikali mauaji hayo ya kinyama ya watu kujichukulia sheria mkononi na kuliagiza Jeshi la polisi wilayani humo kuwasaka watuhumiwa hao na kuhakikisha wanakamtwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
“Naliagiza Jeshi la polisi kufanya msako na kuhakikisha wanawakamata watu watatu ambao ni wa familia moja ambao ndio wanaotuhumiwa na maua ya nwenyekiti ili sheria ichukue mkondo wake,”amesema DC Kasilda
Awali mkuu huyo wa Wilaya amesema sababu za mauaji hayo zinatokana na mgogoro wa ardhi unaowahusisha watuhumiwa hao na serikali ya kijiji.
“Sababu za mauaji hayo ni mgogoro wa ardhi unaowahusisha watuhumiwa hawa wa familia moja, leo(jana) Baraza la ardhi lilienda eneo la mashamba yanayobishaniwa ndipo watuhumiwa walipomvania marehemu na kumkata kata na kitu chenye ncha kali na kisha kukimbia,”amesema DC Kasilda
Alipotafutwa Kamanda wa polisi mkoani humo kuhusiana na mauaji hayo, Simon Maigwa amesema tayari wanamshikilia mtuhumiwa mmoja kwa kuhusika na mauaji hayo na kwamba wanaendelea kuwatafuta watuhumiwa wengine wawili.
“Ni kweli kulitokea mauaji haya ya Mwenyekiti wa kitongoji na tayari tunamshikilia mtuhumiwa mmoja na wengine wawili tunaendelea kuwatafuta ili tuwafikishe kwenye vyombo vya sheria,”amesema Kamanda Maigwa