Arusha. Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), imesema imefunga kwa muda baadhi ya barabara katika hifadhi hiyo kwa ajili ya matengenezo kutokana na kuharibiwa vibaya na nyingine kujaa maji kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumamosi Aprili 27, 2024 na Kaimu Meneja uhusiano wa umma wa mamlaka hiyo, Hamis Dambaya imesema kuwa timu ya wataalamu wa uhandisi inaendelea na kazi ya kurekebisha maeneo yaliyoathiriwa na mvua zinazoendelea kunyesha.
Amezitaja barabara zitakazofungwa kuanzia leo ni ya Ngoitoktok kuelekea msitu wa Lerai kupitia mifupa ya tembo, bakutoka msalama mkubwa kwenda msitu wa Lerai kupitia vumbi la kongoni.
Nyingine ni barabara kutoka Ngoitoktok picnic site kuelekea maeneo maalumu ya kulisha wageni (bush lunch) na barabara ya viboko (hippo pool), kutoka Kijiji cha Endulen kuelekea tambarare za ndutu kupitia Mlima Matiti.
“Mamlaka inapenda kuwatangazia wadau wake hususani madereva wa gari za wageni na waongoza watalii kuwa baadhi ya barabara zitafungwa.”
Aidha eneo la tambarare za Ndutu sehemu kubwa ya ardhi imeshiba maji, hivyo madereva wanashauriwa kutochepuka pembeni mwa barabara kuepuka gari za wageni kukwama,” imesema taarifa hiyo
“Madereva wanasisitizwa kuwa makini katika barabara ya Seneto kuelekea Bonde la Ngorongoro ( entry road) na barabara ya kupanda kutoka kreta ya Ngorongoro (Exit road) ambapo kutokana na ardhi kushiba maji wakati mwingine husababisha maporomoko ya udongo barabarani,” imeongeza.
Taarifa hiyo imesema kuwa timu ya watalii wa uhandisi inaendelea na kazi ya kurekebisha maeneo yote yaliyoathiriwa na mvua zinazoendelea kunyesha, ili kurejesha huduma katika maeneo yote.
Mmoja wa madereva wa magari ya watalii, Chacha Nyandongo ametaja moja ya faida za kufungwa kwa muda kwa barabara hizo ni pamoja na kuweka mazingira salama kwa wageni, kwani kipindi cha mvua baadhi ya barabara hizo huharibika.