Mwanahabari Kabendera aituhumu Vodacom kufanikisha ‘kutekwa’ kwake

Dar es Salaam. Mwanahabari Erick Kabendera ameibua tuhuma nzito dhidi ya kampuni ya huduma za mawasiliano ya simu za mkononi, Vodacom, akiituhumu kuwa ndio iliyofanikisha kukamatwa kwake na askari Polisi, tukio analoliita kutekwa, na kisha kufunguliwa kesi ya uhujumu uchumi, mwaka 2019.

Kutokana na madai hayo, Kabendera ambaye alikuwa amejikita katika uandishi wa habari za uchunguzi, kupitia kwa wakiliwa wake Peter Madeleka ameiandika barua kampuni hiyo akiitaka imlipe fidia ya Dola za Marekani 1 milioni (zaidi ya Sh2.5 bilioni).

“Mteja wetu aliathirika kiuchumi, kijamii na kimaono kutokana na kuwezesha kutekwa kwake. Kwa hiyo tambua kuwa matakwa ya mteja wetu ni kulipwa mara moja Dola za Marekani 1 milioni,” imeeleza barua hiyo ambayo Mwananchi limeiona nakala yake.

Barua hiyo ya Aprili 25, 2024 imebainisha malipo hayo ni fidia ya hasara na madhara mbalimbali alioyapata yakiwamo ya  kiuchumi, yasiyo ya kiuchumi, maumivu ya kiakili na kimaono, kutokufurahia maisha, maendeleo binafsi na hadhi yake katika jamii.

Anaitaka Vodacom kumlipa malipo hayo ndani ya siku 14 kuanzia tarehe ya kuipokea barua hiyo na kama haitafanya hivyo basi wamejiandaa kuchukua hatua za kisheria bila taarifa ya ziada.

Wakili Madeleka aliithibitishia Mwananchi Digital kweli yeye ndiye aliyeandika barua hiyo kwa niaba ya mteja wake Kabendera na tayari walishaiwasilisha Vodacom ambako ilipokewa Aprili 25, 2024.

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Vodacom Tanzania PLC, Zuweina Furaha imeithibitishia Mwananchi Digital leo Jumamosi, Aprili 27, 2024 kuwa kweli wameipokea barua hiyo na wanaifanyia kazi.

“Tumepokea taarifa hiyo na tunaliangalia suala hilo na madai kupitia timu yetu ya wanasheria,” amesema Furaha.

Kabendera ameandika barua ya madai hayo dhidi ya Vodacom, miaka minne baada ya sakata la kesi yake hiyo kumalizika.

Katika barua hiyo Kabendera ameeleza matukio yaliyojiri katika simu yake kabla ya tukio la kukamatwa kwake, kuwa ilianza kupoteza mawasiliano na kumfanya ashindwe kupata huduma ya mawasiliano.

Pia Kabendera ameelezea ili kujua sababu ya tatizo hilo, ilibidi afanye mawasiliano na mwakilishi wa huduma kwa wateja na hata kutembelea ofisi za kampuni hiyo, lakini hakupata ufumbuzi.

Kwa mujibu wa barua hiyo hali hiyo ilianza Julai 27, 2019, saa 9:00 alasiri alipoiwasha simu yake ambayo alikuwa ameizima tangu jana yake usiku na kubaini  haikuwa na mtandao.

Hivyo aliazima simu nyingine akampigia mtoa huduma kwa mteja kujua mazingira yaliyosababisha kumkatia huduma katika simu yake bila kumjulisha kwanza.

Mwakilishi wa huduma kwa wateja wa Vodacom alimweleza kuwa namba yake ya simu ya Vodacom (+255767456796) ilikuwa na changamoto za kiufundi ambayo ilimhitaji kutoa taarifa katika kituo cha huduma kwa wateja cha karibu kilichopo Tegeta.

Kabendera alimtaka mwakilishi huyo kuelezea tatizo ni nini kabla ya kwenda huko kituoni, lakini mwakilishi huyo alikataa akidai ni suala nyeti ambalo linamtaka aende binafsi kituoni hapo.

“Hata hivyo (Kabendera alisita kwenda huko kituo cha huduma kwa wateja) kwa kuwa kulikuwa kuna matukio kadhaa ya watu kutekwa ama kutiwa mbaroni walipokuwa wakitembelea kituo cha huduma kwa wateja tangu mwaka 2016,” inasomeka sehemu nyingine ya barua hiyo na kuongeza:

Jumatatu, Julai 29, 2019 saa 4:00 asubuhi Kabendera alipiga tena simu ya huduma kwa wateja akimlalamikia kuwa alikuwa akihitaji kutoa pesa kwenye simu yake hiyo kwa ajili ya kumnunulia dawa mama yake aliyekuwa mgonjwa.

Mwakilishi wa Vodacom aliyemhudumia alimweleza kuwa asubiri kidogo ili amuulize meneja wake, na alirejea dakika chache baadaye na kumweleza kesi yake ilikuwa nyeti na ilikuwa juu ya uwezo wao kuitatua. 

Badala yake walimshauri atembelee ofisi zao zilizoko Mliman City, Dar es Salaam asubuhi hiyo.

Hata hivyo saa 9:00 alasiri siku hiyohiyo ya Julai 29, ghafla tu simu yake ilianza kufanya kazi, kisha alipopigiwa simu na mwakilishi wa Vodacom ambaye alimtaka (Kabendera) amwelezee tatizo lake na baada ya Kabendera kumuelezea kwa takribani dakika tatu, alikata simu akiahidi kumpigia baadaye kidogo. 

Baada ya takribani dakika tatu Kabendera alipokea simu iliyopigwa kutoka huduma kwa wateja Vodacom ambayo aliipokea akabaini kuwa ilikuwa ni sauti ya mwanaume, ambaye alimtaka Kabendera aeleze mahali alikokuwa na kwamba simu hiyo ilikuwa ikihanikiza na kukwaruza kama vile ilikuwa inarekodiwa.

“Kabla ya simu hiyo kukatwa mteja wetu alimsikia huyo aliyempigia simu hiyo akinong’ona kuwa alikuwa nyumbani kwake na kuongeza kuwa sogea karibu na nyumba yake,” inasomeka sehemu nyingine ya barua hiyo.

Kwa mujibu wa barua hiyo, maelezo hayo yalimstua Kabenderea, na akakimbia sehemu ya juu ya nyumba yake ambako aliweza kuona magari kadhaa ambayo hakuyafahamu, karibu ya nyumba yake. 

Kisha lilitokea gari lingine aina ya Toyota Alphard lililoegesha mbele ya magari hayo upande wa kulia mwa nyumba yake, halafu wakashuka watu wanne ambao walijitambulisha kuwa maofisa wa Polisi lakini walikataa kutoa utambulisho. Walimpiga pingu kumshikilia kizuizini kwa siku mbili.

Barua hiyo inaendelea kueleza wakati wa mahojiano, maofisa wa Polisi walifika katika chumba cha mahojiano wakiwa na karatasi zilizochapishwa kutoka katika kompyuta (printout) za akaunti za pesa ya simu na za namba simu alizokuwa amezipiga kwa mwaka mzima.

Hivyo walimhoji lengo la kila muamala alioufanya kwa mwaka mzima nyuma yake na pia walimhoji uhusiano wake na watu aliokuwa amewasiliana nao miaka kadhaa.

Kabendera analalamika kuwa polisi na Serikali walitoa taarifa kadhaa zenye mgogoro kwa umma kuhusiana na ‘kutekwa’ kwake na kwamba walimtuhumu kwa kutokuwa raia na kumkashifu Rais (wa wakati huo) John Magufuli.

“Hatimaye alishtakiwa mahakamani kwa makosa ya utakatishaji fedha, uhujumu uchumi na ukwepaji kodi na matokeo yake walimuweka chini ya ulinzi mkali katika mahabusu ya gereza la Segerea,” inasomeka taarifa hiyo na kusisitiza:

“Na usikilizwaji wa kesi yake mahakamani uliahirishwa mara 12 upande wa mashtaka ukiomba muda zaidi wa upelelezi”.

Inaeleza zaidi wakati akiwa mahabusu mama yake, Verdiana Mujwahuzi alifariki dunia na hakuruhusiwa kuhudhuria mazishi yake na hata yeye mwenyewe alikuwa na tatizo la kiafya.

Pia inaeleza kutokana na hali hiyo aliamua kukiri makosa na kulipa fidia ya Sh273 milioni ili atoke mahabusu na baada ya kuachiliwa marafiki na familia yake walimweleza kuwa walipigiwa simu na polisi wakiwaonya kutokumtembelea mahabusu, vinginevyo wangepata hatari.

Kabendera baada ya kutiwa mbaroni nyumbani kwake Mbweni Julai 29, 2019, alishikiliwa kwa juma zima, alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Dar es Salaam, Kisutu Agosti 5, 2019 akikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi.

Alisomewa mashitaka matatu ya kupanga na kushirikiana na mtandao wa kiuhalifu.

Mashitaka mengine yaliyomkabili Kabendera ambaye kwa mujibu wa upande wa mashitaka licha ya uandishi wa habari pia ni mfanyabiashara, ni la ukwepaji kodi zaidi ya Sh173 milioni na la utakatishaji fedha zaidi ya Sh173 milioni.

Alidaiwa kuwa katika tarehe tofautitofauti kati ya Januari mwaka 2015 na Julai 2019, alitenda kosa la kutoa msaada kwa genge la uhalifu kwa nia ya kujipatia masilahi.

Katika shitaka la pili la ukwepaji kodi, alidaiwa kuwa katika tarehe tofautitofauti kati ya Januari 2015 na Julai 19, 2019, mshtakiwa huyo alishindwa kulipa kodi kiasi cha Sh173.24 milioni.

Katika shitaka la tatu la utakatishaji fedha alidaiwa kuwa katika tarehe tofautitofauti, kati ya Januari 2015 na Julai 2019, katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam, alitakatisha fedha kiasi cha Sh173.24 milioni.

Alidaiwa kuwa kosa hilo huku akijua kuwa pesa hizo ni mazao ya uhalifu wa kukwepa kodi na kushiriki kupanga uhalifu.

Hata hivyo Kabendera aliachiliwa huru Februari 24, 2020 baada ya kufanya majadiliano kufikia makubaliano na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), ya kukiri makosa yaliyokuwa yanamkabili.

Katika makubaliano hayo alifutiwa shitaka moja la uhalifu wa kupanga na kubakiwa  na mashaka mawili ya kukwepa kodi na utakatishaji fedha, ambayo aliposomewa tena mahakamani alikiri.

Alipoulizwa na Hakimu Agustine Rwizile kama iliingia katika makubaliano hayo  kwa hiari yake alikiri kuwa ni hiari yake na hakulazimishwa.

Kutokana na kukiri huko Mahakama ilimtia hatiani na kumuhukumu adhabu ya kulipa faini ya Sh250,000 au kifungo cha miezi mitatu jela akishindwa faini kwa kosa la kwanza la kukwepa kodi.

Pia kwa kosa hilohilo mahakama hiyo ilimuhukumu adhabu ya kulipa fidia ya hasara aliyoisababisha, yaani kiasi cha kodi aliyokwepa Sh173.24 milioni.

Kwa kosa la pili (utakatishaji) ilimuhukumu adhabu ya kulipa faini ya Sh100 milioni kwa mujibu wa makubaliano baina yake na DPP na kwamba adhabu zote zinakwenda kitofauti (haziendi kwa pamoja bali kila moja inajitegemea).

Kabendera alilipa  faini hizo Sh100 milioni ambazo alikuwa amekwishazilipa kabla ya makubaliano hayo kufikishwa mahakamani na Sh250,000 alizozilipa baada ya makubaliano kufikishwa mahakamani,  hivyo akaachiwa huru.

Related Posts