Dar es Salaam. Jeshi la Polisi nchini Tanzania limewataka watu wenye taarifa tofauti juu ya ajali ya bodaboda iliyotokea alfajiri ya jana Ijumaa Aprili 26, 2024, eneo la Makonde, mkoani Dar es Salaam na kusababisha kifo cha Noel Mwingira, maarufu Zuchy wazipeleke zifanyiwe kazi.
Katika ajali hiyo, dereva bodaboda ambaye jina bado halijafahamika alijeruhiwa na kupelekwa hospitalini. Ajali hiyo imeibua mijadala mitandaoni ikiwemo lawama kwa Jeshi la Polisi ikidaiwa kuwa lilichelewa kufika eneo la tukio kutoa msaada ambapo wananchi walipiga kuomba msaada wakajibiwa kuwa gari halina mafuta.
Kutokana na mjadala huo, Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, David Misime jana Ijumaa Aprili 26, 2024 ametoa taarifa kwa umma kuhusu tukio hilo akianza kwa kusema: “Kwanza, Jeshi la Polisi linasema hili ni tukio la huzuni na la kusikitisha kwa sababu tumempoteza Mtanzania mwenzetu katika ajali hiyo.”
Katika taarifa hito Misime amesema tukio hilo liliripotiwa saa 10:12 alfajiri kuwa kuna ajali imetokea eneo la Mbezi Makonde. Baada ya kupokelewa taarifa hiyo maofisa na askari waliokuwa kwenye majukumu katika mkesha wa Tamasha la Shangwe la Utawala, lililokuwa linafanyika eneo la Tanganyika Packers waliondoka wakiwa na gari ya Polisi kuelekea eneo la tukio.
Amesema baada ya kufika waliuchukua mwili na kuupeleka Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala kwa taratibu nyingine za kisheria.
Misime amesema askari waliofika eneo la tukio katika uchunguzi imebainika marehemu alipata ajali na pikipiki aliyokuwa amepanda yenye namba MC 436 CMU iliyokuwa ikiendeshwa na dereva ambaye alipata majeraha na anaendelea na matibabu.
“Hivyo, baada ya taarifa ya tukio hilo kutolewa na kupokelewa, maofisa na askari polisi walifika kwenye tukio kwa wakati na kutekeleza yale yanayopaswa kutekelezwa kwenye eneo la ajali. Tunawashukuru bodaboda wa eneo hilo wanaojali utu wa binadamu kwa kuzuia magari yasimkanyage marehemu,” imesema sehemu ya taarifa iliyosainiwa na Misime na kufafanua kuwa.
“Endapo kuna mwenye taarifa tofauti na si za uzushi/uwongo kama hizo zinazosambazwa azifikishe kwa viongozi ili zifanyiwe kazi na hatua zichukuliwe.”
Taarifa ambazo Mwananchi Digital limezipata, msiba wa Zuchy upo Chanika, jijini Dar es Salaam na taratibu za mazishi zinaendelea.
Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi.