Dar es Salaam. Rais Samia Hassan Suluhu ametoa msamaha kwa wafungwa 1,082, ikiwa ni katika kuadhimisha miaka 60 ya Muungano wa Tanzania.
Rais Samia ametoa msamaha huo kwa kutumia mamlaka aliyopewa chini ya Ibara ya 45(1)(a)-(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kutoa msamaha kwa wafungwa kwa masharti maalumu.
Taarifa hiyo imetolewa leo Jumamosi, Aprili 27,2024 na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni.
Taarifa hiyo imesema kati ya wafungwa hao waliosamehewa, 29 wameachiliwa huru tangu jana Aprili 26,2024.
Wakati wafungwa 20 waliohukumiwa adhabu ya kifo wamebadilishiwa adhabu hiyo kuwa kifungo cha maisha na wafungwa 27 waliohukumiwa kifungo cha maisha wamebadilishiwa adhabu na kuwa kifungo cha miaka 30.
Huku wafungwa 1,006 wamepunguziwa adhabu zao na watabaki gerezani na kuendelea na sehemu ya kifungo kilichobaki.
“Msamaha huu unawahusu wafungwa ambao wamehukumiwa kifungo cha kuanzia miaka miwili na kuendelea na ambao tayari wametumikia robo ya adhabu zao gerezani na wawe wameingia gerezani kabla ya Desemba 2023,”imesehema sehemu ya taarifa hiyo.
Kigezo kingine ni wafungwa wagonjwa wenye magonjwa ya kudumu au sugu ambao wapo kwenye hatua za mwisho na ugonjwa na hatua hiyo ithibitishwe na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa au Mganga wa Wilaya.
Wafungwa wengine ni wale wanaotumikia kifungo cha maisha gerezani ambao wametumikia adhabu zao kwa miaka 15 na kuendelea wamebadilishiwa adhabu zao kuwa kifungo cha miaka 30.
Wapo pia wafungwa wa kunyongwa waliomaliza taratibu za kimahakama ambao wamekaa gerezani kwa muda wa miaka kumi na kuendelea, ambao wamebadilishiwa adhabu hiyo na kuwa kifungo cha maisha.
“Wafungwa waliowahi kubadilishiwa adhabu kwa msamaha wa Rais kutoka adhabu ya kifungo cha maisha ambao wametimiza miaka kumi na kuendelea tangu kupata msamaha huo, wamebadilishiwa kifungo cha maisha kuwa kifungo cha miaka 30,”imeeleza taarifa hiyo.
Pia wapo wafungwa wazee wenye umri wa miaka 70 au zaidi , umri huo uthibitishwe na japo la waganga chini ya uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya.
Msamaha huu unawahusu wafungwa wa kike walioingia na ujauzito gerezani au wenye watoto wanaonyonya na wasionyonya.
“Wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili wasio na uwezo wa kufanya kazi, ulemavu huo uthibitishwe na jopo la waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa au Mganga Mkuu wa Wilaya.”
“Msamaha huu unawahusu wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kuwekwa kizuizini ambao wamekaa gerezani kuanzia miaka kumi au zaidi.
“Ni matarajio ya Serikali kuwa wafungwa walioachiwa huru watarejea tena katika jamii kushiriki na wananchi wenzao katika ujenzi wa Taifa letu na kujiepusha kutenda makosa ili wasirejee tena gerezani,”imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Wafungwa wasiohusika na msamaha huo
Hata hivyo, taarifa hiyo imesema kuwa msamaha huo hautawahusu wafungwa wanaotumikia vifungo vya nje na wale waliowahi kukiuka masharti ya vifungo vya nje chini ya sheria ya Bodi za Parole sura ya 400(R.E) 2002.
Wengine ni wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo gerezani ambacho siyo cha maisha kwa makosa ya uhujumu uchumi, matumizi mabaya ya madaraka , utakatishaji wa fedha , rushwa, usafirishaji au kujihusisha kwa namna yoyote na dawa za kulevya ikiwemo bangi.
“Wafungwa waliopatikana na hatia ya kuhukumiwa kifungo gerezani ambacho sio cha maisha kwa makosa ya kukutwa na viungo vya binadamu, unyang’anyi wa kutumia nguvu, unyang’anyi wa kutumia silaha , kumiliki silaha au ktenda makosa hayo,”imeeleza sehemu ya taarifa hiyo ikifafanua zaidi.
“Wafungwa wanaotumikia kifungo gerezani ambacho siyo cha maisha kwa makosa ya kujihusisha kwa namna yoyote ile na nyara za Serikali, ujangili, makosa ya wizi au ubadhilifu wa fedha za Serikali,”imeeleza taarifa hiyo.
Pia msamaha huu hautawahusu wafungwa wanaotumikia vifungo gerezani kwa makosa ya kutoroka au kujaribu kutoroka chini ya ulinzi halali au kusaidia kutendeka kwa makosa hayo.
Wafungwa wenye makosa ya kujaribu kuua, kujiua au kuua watoto wachanga, ugaidi, uharamia na makosa ya kimtandao hawatahusika pia.
Wafungwa warudiaji na wale waliowahi kupata msamaha wa Rais , watenda makosa ya kinidhamu gerezani ambao makosa hayo hajayatimiza miaka mitatu mpaka kufikia Aprili 26,2024 na wafungwa wa madeni, pia hawahusiki na msamaha huo.