BAADA ya kufunga bao pekee katika mchezo wa fainali ya Kombe la Muungano, kiungo wa Simba Babacar Sarr ameiwezesha timu hiyo kuvuna kitita cha Sh50 milioni ambayo ni zawadi ya mshindi ya bingwa.
Sarr alifunga bao hilo kwa kichwa katika dakika ya 77 akiunganisha mpira wa faulo uliopigwa ikiwa ni matokeo ya madhambi yaliyofanywa na Azam karibu na mstari wa katikati ya uwanja.
Mbali ya kupoteza mchezo Azam ilionekana kuchangamka zaidi kipindi cha pili cha mechi ambapo ilifanya mashambulizi kadhaa kwa Simba, lakini hayakuzaa matunda.
Hii inakuwa ni mara ya sita kwa Simba kuchukua ubingwa wa michuano hii ikiwa imeifikia Yanga ambayo pia imechukua mara sita.
Michuano hiyo ambayo imefanyika Uwanja wa Aman, Zanzibar, imerejea kwa mara ya kwanza baada ya kusimama kwa takribani miaka 20 ambapo awali ilikuwa ikishirikisha timu nane ikiwa ni nne kutoka Bara na nne Zanzibar, lakini sasa limerudi na timu nne.
Simba ilifika fainali baada ya kuichapa KVZ kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na straia wao Fredy Michael na beki Israel Mwenda, wakati Azam ikifika kwa kuiondosha KMKM kwa kichapo cha mabao 5-2.
Mbali ya zawadi ya mshindi wa pili, Azam ambayo imeshiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza pia imejizolea Sh30 milioni.
Baada ya mchezo nahodha wa Simba, Mohamed Hussen alisema: “Nawapongeza Azam wana timu nzuri, lakini pia niwapongeze wachezaji wenzangu kwa sababu walipambana vya kutosha. Haikuwa fainali rahisi ndio maana unaona tumepata ushindi wa bao moja.”
Kwa upande wa Azam, nahodha Yahya Zayd amewapongeza Simba kwa ubingwa na kusema wao wamekubaliana na kile kilichotokea na wanaangalia mbele.