Dar/mikoani. Mvua zinazoendelea kunyesha katika mikoa mbalimbali, zimeendelea kuleta madhara ikiwemo kusababisha vifo vya watu wanne wa familia moja na kukata mawasiliano ya upande mmoja kwenda mwingine.
Mwenendo wa hali ya mvua unadaiwa kusababisha vifo vya watu wanne familia moja wanaoishi Mtaa wa Goroka Tuangoma wilayani Temeke, Dar es Salaam waliodondokewa na ukuta wa nyumba iliyokuwa ikijengwa karibu na makazi yao.
Tukio hilo lililitokea juzi asubuhi ambapo Lidya Heza (21), Agnes Eliya (20), Stella Rujukundi (20) na Joyce Rujukundi (12), walifariki dunia huku wengine saba wakinusurika katika tukio hilo.
Mvua iliyonyesha ilisababisha ukuta wa nyumba hiyo ya jirani kuangukia kwenye chumba walicholala watu watano kati yao ni hao wanne waliofariki huku Rechael Rujukundi (9) anayesoma darasa la nne shule ya Goroka akinusurika.
Akizungumzia tukio hilo jana, Mariamu Julius ambaye ni mama wa familia hiyo amesema walionusurika walikuwa wamelala vyumba vya jirani.
“Katika nyumba yangu hii iliyobomoka ilikuwa na vyumba vitatu na siku ya tukio ukuta uliangukia katika chumba walicholala mabinti zangu watano, lakini Rechael amepona baada ya kukutwa juu ya chandarua wakati wa uokoaji,” amesimulia.
Amesema katika vyumba hivyo chumba kimoja alikuwa amelala yeye na mumewe Sayon Rujukundi ambaye siku hiyo aliwahi kutoka kwenda kazini.
“Chumba kingine walilala watoto wanne wa kiume, wawili kati yao ni watoto wangu wengine walikuwa ni rafiki zao ambao huwa wanasoma nao,” amesema
Mariamu amesema katika hao wanne waliofariki wawili ni watoto wake wa kuwazaa ambao ni Stella na Joyce lakini waliobakia ni watoto wa dada zake waliokuja kuwasalimia kutoka mkoani Kigoma.
Mariamu siku hiyo alikwenda kuwasalimia wote walikuwa wazima wa afya lakini Stella alimueleza kuwa usiku wa kuamkia siku hiyo hawakulala.
“Aliniambia aliota njozi kwamba ukuta umewabomokea, niliwaambia poleni Mungu ametulinda tumshukuru maana tupo salama, lakini kitendo cha kutoka chumbani kwao nilisikia kishindo kikali nyuma kama radi kugeuka ukuta umewafunika,” amesema.
Mariamu amesema alilia na kuanza kuita majirani kuja kutoa msaada wa kuwaokoa ambapo walijitokeza kwa wingi lakini walifanikiwa kumuokoa mtu mmoja pekee.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, amekiri kutokea tukio hilo huku akieleza alikwenda kushirikiana na familia kuchukua miili kuipeleka mochwari ya Polisi Barracks Kurasini na mazishi yatafanyika leo.
“Serikali tumetoa majeneza yote manne na tumetoa ubani kidogo wa kusaidia shughuli ya mazishi,” amesema Mapunda
Mapunda amesema tukio hilo limesababishwa na kudondokewa na ukuta wa nyumba iliyojengwa jirani na nyumba waliyokuwa wanaoishi watoto hao.
“Kulikuwa na mtu aliyejenga nyumba juu kutokana na jiografia yake kuna kimlima hivi na huyo mtu alikuwa haishi hapo aliondoka muda mrefu sasa kutokana na mvua hizi ikadondokea nyumba waliokuwamo watoto hawa,”
Mapunda amewataka wananchi kuzingatia tahadhali zinazotolewa na mamlaka husika kuhusu mwenendo wa mvua na kutoa ruhusu watoto kwenda shuleni wakiona inanyesha kubwa.
“Wakiona mvua kubwa na watoto wako shule basi wasiwaache warudi peke yao wawafuate wawasaidie katika hizo nyakati,” amesema.
Tangu mvua za El-Nino zilipoanza Oktoba mwaka jana zimesababisha vifo vya watu zaidi ya 162 katika maeneo mbalimbali nchini.
Mamia ya wananchi walisota kwa takribani saa 20 kutokana na daraja la Kifaulongo katika Kata ya Tambani mkoani Pwani kukatika na kusababisha adha kwa watumiaji wa eneo hilo.
Daraja hilo lilikatika saa moja usiku wa kuamkia leo Aprili 27,2024 mvua zilizokuwa zimenyesha maeneo mbalimbali ya mikoa ya Pwani na Dar es Salaam.
Hatua hiyo ilisababisha kina mama wenye watoto wakihangaika kutaka kuvuka kwenye maji ili kwenda upande wa Mbande, Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam kupata huduma za afya.
Wananchi hao walilazimika kuweka magogo, ngazi na kuvushana kwa wanaoweza, huku wengine wakinusurika kusombwa na maji.
Hata hivyo, baadaye walioruhusiwa kupita ni wenye dharura za msingi ili kuepusha maafa zaidi.
Mkazi wa Tambani Shule, Adelina Kisaka amesema alifika hapo tangu saa 12 asubuhi akitaka kwenda kumpeleka mtoto wake hospitali, lakini alikwama kutokana na kukatika daraja hilo.
Amesema kulikuwa na vijana waliojitolea kwa kuweka daraja hata hivyo, alishindwa kuvuka kwa kuhofia usalama wake na mtoto wake.
“Nimekuta vijana wamejitolea wanavusha watu kwa Sh1,000 nilishindwa kwa sababu hata eneo lenyewe walilolaza ngazi linakaribia kuanguka,” amesema Kisaka.
Mkazi mwingine wa eneo hilo, Khamis Kato amesema ndugu zao na jamaa walishindwa kushiriki msiba ambao upo nyumbani kwao Kijiji cha Mkoga.
“Huu msiba umetokea tangu jana (juzi) hata hivyo gari lililobeba waombolezaji kutoka Kigamboni lilikwama darajani, tunaangalia namna nyingine ya kuzunguka ili kuwahi mazishi.”
Adha hiyo ilimfikisha eneo hilo, Mbunge wa Mkuranga, Abdallah Ulega kujionea hali ilivyo na kuwapa pole wananchi aliowahidi kujengwa kwa daraja la muda.
Akizungumza na wananchi, Ulega amesema Serikali imechukua hatua za dharura ikiwamo kuagiza lijengwe daraja la muda kwa kujaza mawe eneo lililokatika kisha kuwekwa daraja la mbao.
“Ninawapa pole wananchi waliokumbwa na kadhia na hadi kufikia saa 10 jioni leo (jana) ninaamini mawasiliano yatarejea,” amesema.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mkoga, Amani Kamwaga amesema wamepokea maagizo ya mbunge na utekelezaji umeanza.
Alisema Ulega alichangia Sh300,000 kwa ajili ya kununua mbao zitakazotumika kutengenezea daraja la muda.
“Muda huu kuna vijana wamejitolea kuvusha wananchi kwa gharama ya Sh200 hadi Sh500 lakini hadi jioni tukikamilisha hawataendelea kuwatoza fedha wananchi,” amesema.
Katika hatua nyingine Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), imefunga kwa muda baadhi ya barabara katika hifadhi hiyo ili kupisha matengenezo baada ya kuharibiwa vibaya na mvua zinazoendelea kunyesha.
Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Kaimu Meneja uhusiano wa umma wa NCAA, Hamis Dambaya, ilieleza timu ya wataalamu wa uhandisi inaendelea na kazi ya kurekebisha maeneo yaliyoathirika.
Dambaya alizitaja barabara zilizofungwa ni pamoja Ngoitoktok kuelekea msitu wa Lerai kupitia mifupa ya Tembo,barabara kutoka Msalama mkubwa kwenda msitu wa Lerai kupitia vumbi la Kongoni.
Nyingine ni Ngoitoktok Picnic site kuelekea maeneo maalumu ya kulisha wageni (bush lunch) na barabara ya viboko (hippo pool), barabara kutoka Kijiji cha Endulen kuelekea tambarare za ndutu kupitia mlima Matiti.
“Mamlaka inapenda kuwatangazia wadau wake hususani madereva wa magari ya wageni na waongoza watalii kuwa baadhi ya barabara zitafungwa,”amesema.
Dambaya amesema eneo la Tambarare za Ndutu sehemu kubwa ya ardhi imeshiba maji,hivyo madereva wanashauriwa kutochepuka pembeni mwa barabara ili kuepuka gari za wageni kukwama.
“Madereva wanasisitizwa kuwa makini katika barabara ya Seneto kuelekea Bonde la Ngorongoro (entry road) na barabara ya kupanda kutoka kreta ya Ngorongoro (Exit road) ambapo kutokana na ardhi kushiba maji wakati mwingine husababisha maporomoko ya udongo barabarani,” alisema.