Songwe. Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo amemuagiza Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani humo, kufanya uchunguzi wa matumizi ya fedha kwenye ujenzi wa bweni la wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika shule ya msingi Ipapa iliyopo wilaya ya Ileje kwa gharama ya zaidi ya Sh100 milioni.
Chongolo ametoa agizo hilo leo Aprili 28, 2024 wakati akikagua ujenzi wa mradi huo ambao ulianza kujengwa tangu mwaka 2022 na hadi sasa haujakamilika.
Amesema taarifa za ujenzi wa mradi huo ambao unatarajia kuwanufaisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu zaidi ya 300, hazina ukweli kutokana na kukinzana kwa viongozi kuhusu uagizwaji wa vifaa ambavyo wamedai ndiyo chanzo cha kuchelewa kwa mradi.
Amesema licha ya fedha hizo kutolewa na Serikali Kuu, bado hakuna makadirio mazuri kutoka kwa wataalamu wa ujenzi kuhusu gharama za kumalizia mradi, ambao ungetatua changamoto ya watoto wenye mahitaji maalumu ambao wanatarajia kuanza kulitumia bweni hilo.
“Naomba mnieleze sababu za msingi za kuchelewa kwa mradi huu, lakini nasikitika jengo hili kujengwa kwa mifuko ya saruji zaidi ya 900, kwa kweli mmenishangaza sana, nawasihi simamieni nafasi zenu,” amesema Chongolo.
Baada ya maelezo hayo, Chongolo ameagiza kuanzia leo Aprili 28, 2024 mpaka Juni 15, 2024, mradi huo ukamilike na uanze kufanya kazi huku Takukuru wakifanya uchunguzi wa kina kuhusu matumizi ya fedha hizo.
Akizungumza mbele ya mkuu huyo wa mkoa, diwani wa kata hiyo, Gwalusako Kapesa amesema mradi huo umechelewa kwani wataalamu wanadai mifumo ya manunuzi kuwa migumu kuagiza vifaa vya ujenzi, ameomba uwekwe mfumo wa Serikali iweke utaratibu mzuri wa uag izaji wa vifaa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Nuru Kindamba ameahidi kukamilisha mradi kwa muda uliotolewa na mkuu wa mkoa kwani tayari wametenga milioni 40 kutoka mapato ya ndani kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa bweni hilo.