Na Janeth Raphael -MichuziTv -Dodoma
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt Dotto Biteko anatarijiwa kuwa Mgeni Rasmi katika Mkutano wa 13 wa Kitaaluma wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) utakaofanyika Jijini Dodoma tarehe 29 na 30 April 2024.
Taarifa hiyo imetolewa mapema leo Jijini Dodoma na Neville Meena ambaye ni Mwandishi wa Habari na Mjumbe kamati ya Utendaji Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) katika mkutano wake na Waandishi wa habari wakati akielezea kufanyika kwa mkutano huo ambao utahudhuriwa na jumla ya Wahariri 150 kutoka vyombo mbalimbali vya Habari hapa Nchini na uliobeba Kauli mbiu inayosema:Nafasi ya Vyombo vya Habari katika Matumizi ya Gesi,Kwaajili ya Kulinda Misitu.
“Tutakuwa na mkutano wa kitaaluma wa 13,mikutano hii ya kitaaluma huwa inajadili mada Mahsusi kwa wakati huo. Sisi tumeanza miaka 14 iliyopita lakini kuna mwaka mmoja mkutano haukufanyika kutokama na mazingira kutoruhusu.
Mkutano huu utafanyika hapa Dodoma na utashirikisha wahariri wapatao 150 kutoka vyombo mbalimbali vya habari hapa Nchini,lakini vyombo hivyo vingi viko Dar es Salaam “.
“Mkutano tutaanza asubuhi na mada zetu za ndani na Mchana utafunguliwa na Mgeni Rasmi ambaye ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri Nishati Mhe Dkt Dotto Biteko na pia Tunatarajia kwamba Waziri wetu wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye atakuwepo”.
“Sasa mada kuu ama kaulimbiu inayoongoza mkutano wetu ni:”Nafasi ya vyombo vya habari katika matumizi ya Gesi,kwaajili ya kulinda Misitu” hii ndio kuu ambayo tumekuja nayo katika wetu wa kesho na keshokutwa”.
Aidha Meena amesema kuwa katika mkutano huo kutakuwa na mada mbalimbali za kitaaluma ambazo wanapaswa kuzijadili wao waandishi wa habari ikiwemo nafasi za wanawake katika vyumba vya habari lakini pia kuangazia masuala ya Uchaguzi ulioko mbele yetu kama vile uchafuzi wa Serikali za mitaa kwani waandishi wa habari ni wahusika wa masuala ya uchafuzi.
“Tutakuwa na mada zingine za kitaaluma zinazohitaji tuzijadili kama waandishi wa habari kama vile nafasi za wanawake katika vyumba vya habari,haki zao,wajibu wao pamoja na uzingatiaji wa Taaluma. Tutakuwa na Mada kuhusiana na Uchaguzi,kama mnavyofahamu mwaka huu kuna uchaguzi wa Serikali za Mitaa,kwasababu tunahusika na masuala ya uchaguzi hivyo ni vema tukajiandaa kuhusiana na jambo hilo”.
Naye Salim Saidy Salim mjumbe wa Kamati ya Utendaji Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) ametua nafasi hii kuwakumbusha Waandishi wa habari wawe wenye kuandika Habari za misitu na kufuatilia maendeleo yake na sio kutoa taarifa wakati wa kupandwa tu.
“Kwa mfano nawalaum sana Waandishi wa habari,ninyi vijana wangu mko hodari kuandika misitu wakati wa kupanda misitu kwa kusema kiongozi fulani kaongoza upandaji miche 1000 na mengineyo,lakini hatufanyi mwendelezo wa ufuatiliaji wa ile misitu tuliyopanda kwa kujua mungapi imeendelea kuwa hai,juhudi gani zinafanyika ili kulinda na kuelezea athari za kutokuwa na Misitu”.
Pia Salim ameamalizia kwa kukumbushana kuhusu suala la mavazi kwa Waandishi wa Habari Wanawake na Wanaume kuwa nadhifu wakati wote lakini hasa wanapokuwa katika Mikutano ya ki Habari.
Huu ni mkutano wa 13 ambao utahudhuriwa na jumla ya Wahariri 150 kutoka vyombo mbalimbali hapa Nchini waliopo chini ya Jukwaa la wahariri TEF.