Hatima ya vigogo Tume Huru ya Uchaguzi kuteka bajeti ya Sheria na Katiba

Dodoma. Hoja ya kuwataka wajumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kujiuzulu, vyama kuanzisha madawati ya jinsia na Katiba mpya, huenda zikapata majibu katika hotuba ya bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria.

Mbali ya hayo, ni utekelezaji wa falsafa ya Rais Samia Suluhu Hassan ya R4, yaani maridhiano, ustahimilivu, mageuzi na kujenga upya.

Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2022/2023 iliomba kuidhinishiwa na Bunge Sh383.619 bilioni ikiwa na vipaumbele 30, ikiwamo kuratibu mchakato wa Katiba mpya, kutekeleza mkakati wa kutoa elimu ya Katiba kwa umma, kutekeleza kampeni ya Mama Samia Legal Aid kwa wananchi kote nchini.

Vipaumbele vingine ni kufanya marekebisho ya sheria za uchaguzi na demokrasia, kutekeleza programu ya kutumia lugha ya Kiswahili katika utoaji haki nchini, kuendelea kuimarisha mifumo ya utoaji haki ili haki ipatikane kwa wote, na kwa wakati na kuimarisha mifumo ya utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala kwa kuanzisha na kuendesha kituo cha kimataifa cha utatuzi wa migogoro.

Macho na masikio ya wadau

Kesho, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Pindi Chana atawasilisha bungeni hotuba ya bajeti ya wizara kwa mwaka wa fedha wa 2024/25.

Miongoni mwa hoja ambazo wadau wa siasa wanasubiri kusikia majibu yake ni baada ya Serikali kutangaza mabadiliko ya jina la Tume ya Uchaguzi kuwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi,  huku wadau, wakiwamo viongozi wa vyama vya siasa wakitaka mabadiliko hayo yaendane na mabadiliko ya muundo kwa mujibu wa Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na.2 ya 2024.

Sheria hiyo ni miongoni mwa tatu zilizotiwa saini na Rais Samia Suluhu Hassan, zikiwamo Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024 na Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2024.

Kwa mujibu wa tangazo la Serikali Na.225 la Machi 29, 2024, mabadiliko ya jina la tume ya uchaguzi kuwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi yalianza kutumika Aprili 12, 2024.

Tangazo hilo liliwaibua wadau, wakiwamo viongozi wa vyama vya siasa wakitaka mabadiliko yaendane na utekelezwaji wa sheria yote ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, ikiwemo kuwapata wajumbe wapya wa Tume.

Mbali na hoja hiyo, waziri mwenye dhamana huenda akatoa majibu kuhusu uanzishwaji wa dawati la jinsia ndani ya vyama vya siasa.

Hoja hiyo ilitolewa na mbunge wa Viti Maalumu, Neema Lugangira alipochangia mjadala wa makadirio ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge.

Lugangira alisema miongoni mwa vipengele kwenye muswada wa mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa ni vyama hivyo kuanzisha madawati ya jinsia yatakayoshughulikia matatizo ya unyanyasaji wa wanawake wanaojitosa kwenye siasa.

Mbali na Lugangira, Kiongozi wa Chama cha ACT- Wazalendo, Dorothy Semu  aliwahi kunukuliwa na Mwananchi akisema kutangazwa kwa jina jipya ni hatua moja, ila wanaitaka Serikali iendelee kutekeleza yaliyomo kwenye sheria, ikiwemo kuwapata wajumbe wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi.

“Hivyo, tunategemea sheria ya usimamizi wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa italetwa haraka iwezekanavyo na mengine ambayo Tume imepewa mawanda ya usimamizi wa sheria, ikiwemo kupata makamishna wapya wa tume kwa njia ya kutangazwa na kusailiwa,” alisema.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika akizungumzia mabadiliko ya jina hilo, alisema yalipaswa kuanzia kwenye mabadiliko ya Katiba.

Mnyika amesema kwa mujibu wa Katiba, uamuzi wowote unaofanywa na tume hiyo hauwezi kuhojiwa na kama mtu anataka kuyapinga apinge uchaguzi, jambo alilosema linaifanya tume isiwe huru.

Kwa mujibu wa Mnyika,  tume ni ya Serikali, kwani wadau hawana uwakilishi ndani yake na hata uundwaji wake kwa muswada uliopo ni danganya toto.

“Muswada wa sasa ni sheria ambayo ni danganya toto, wamesema kutakuwa na kamati ya uteuzi kabla tume haijateuliwa, lakini hiyo kamati ni ya kina nani? Ni Jaji Mkuu wa Muungano, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mwenyekiti wa Tume ya Haki na Utawala Bora na makamu wake kwa upande wa Zanzibar? Kwa hiyo kwa misingi hii ni Tume ya Rais,” amesema Mnyika.

Amesema kwa Katiba iliyopo matokeo ya urais hayawezi kuhojiwa mahakamani, hivyo hata tume ikiwa bora kiasi gani itafanya vurugu zote, lakini matokeo ya urais hakuna pa kukimbilia.

Amesema Katiba ya sasa inaelekeza watumishi wa umma na haijaweka utaratibu wa tume kuajiri watumishi wake, hivyo itakuwa ikiamua aina ya watumishi wa umma kusimamia uchaguzi.

Waziri Dk Chana kwenye hotuba yake ya bajeti huenda akajibu hoja za wanasiasa kwamba kifungu cha 27 cha sheria hiyo, kinatoa mwanya kwa tume kutumia wakurugenzi wa halmashauri na watendaji kusimamia uchaguzi.

Pia, Kiongozi mstaafu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, aliandika katika ukurasa wake wa X, akisema: “Kwa kuwa Sheria mpya ya Tume Huru ya Uchaguzi imeanza kutumika na kwa kuwa makamishna wa tume wanaohudumu walipatikana kabla ya sheria hii na kwa mazoea tu (hapakuwa na Sheria ya Tume ya Uchaguzi kabla ya sasa), tunawasihi wajumbe wa Tume ya Uchaguzi waliopo wajiuzulu.”

Waziri Chana pia anatarajiwa kutoa majibu kuhusu hoja ya daftari la wapigakura liwe moja kwamba litumike pia kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa.

Related Posts