Kocha wa Fei Toto afariki dunia

KOCHA wa zamani wa Feisal Salum ‘Fei Toto’, Salum Khatib amefariki dunia baada ya kugongwa na gari akitokea mazoezini kuinoa timu ya JKU SC na anatarajiwa kuzikwa mchana wa leo katika makaburi ya Mwanakwerekwe, Zanzibar.

Khatib enzi za uhai wake akiwa kocha wa timu JKU, alimfundisha kiungo wa sasa wa Azam FC, Fei Toto na wa Yanga, Shekhan Ibrahim Khamis na hadi umauti unamkuta alikuwa kocha wa timu hiyo ya Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar.
 
Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Mkuu wa JKU, Salum Haji amesema wamempoteza kocha na kiongozi ndani ya timu yao huku akikiri kuwa licha ya udogo wa nafasi ndani ya timu hiyo yeye ndiye alikuwa kocha kiongozi kwasababu alikuwa mkubwa kiumri kuliko makocha wote wa benchi la ufundi.

“Kocha tulikuwa naye katika mazoezi asubuhi, na aliniambia mchana ataenda Donge nje ya mji na kwamba mchana akirudi tutazungumza, sio bahati mbaya tuseme nzuri kwasababu Mungu kampenda zaidi na kwake sote tutarejea,” alisema na kuongeza:

“Hakika mauti ni mawaidha kwetu kuna jambo la kujifunza, yapo mambo hatutayasahau kamwe kwenye maisha yetu, amenifanya niwe kocha mkuu, kanifunza mambo mengi, alikuwa mtu wa kutimiza mambo kila tulilokuwa tunapanga, alikuwa anahakikisha linatimia,” amesema.

Haji amesema wamepoteza mtu muhimu kwenye timu yao kutokana na namna walivyokuwa wanaishi naye ikiwa ni pamoja na kuwajenga wachezaji kuamini katika kupambana.

“Mwenyezi Mungu ampe nuru ya kaburi, ampokee akiwa amemridhia, ampe kitabu chake kwa mkono wa kulia, alijaalie kaburi lake kuwa miongoni mwa bustani za Peponi na ampe kivuli siku ya Kiama,” amesema.

Related Posts