Ni fursa nzuri kwa Pamba kumaliza unyonge wa miaka 22 wa kukaa bila kushiriki Ligi Kuu itakapokabiliana na Mbuni FC kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha kuanzia saa 10 jioni, leo.
Ushindi katika mechi hiyo utaifanya Pamba ambayo mara ya mwisho kushiriki Ligi Kuu 2002, kuchukua nafasi moja iliyobaki katika Ligi ya Championship ya kwenda katika daraja hilo la juu la ligi nchini kwani itafikisha pointi 67 ambazo hazitaweza kufikiwa na timu nyingine yoyote kati ya 14 zilizo chini yake.
Lakini hata matokeo ya sare yanaweza kuivusha Pamba kwani yataifanya ifikishe pointi 65, lakini itapaswa kuombea Mbeya Kwanza inayocheza na Transit Camp kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona Mtwara isipate ushindi wa kuanzia mabao 13 ili yenyewe ipande Ligi Kuu Bara.
Lakini kama Pamba itapoteza, Mbeya Kwanza inaweza kupata fursa hiyo ikiwa itapata ushindi dhidi ya Transit Camp na maana yake itakuwa inarejea Ligi Kuu baada ya kushuka msimu wa 2021/2022.
Vita kubwa itakuwa baina ya FGA Talents, Stand United na Green Warriors ambazo kila moja inapambana isimalize katika nafasi nne za kucheza mechi za mchujo kuwania kubaki Championship.
FGA Talents iko nafasi ya 10 ikiwa na pointi 31 sawa na Stand United, lakini inanufaika na utofauti mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa wakati Green Warriors iko nafasi ya 12 ikiwa na pointi 28.
Tayari timu ya KenGold imepanda Ligi Kuu huku timu ya Ruvu Shooting ikiwa imeshashuka daraja na leo itaungana na timu nyingine moja ambayo itashuka moja kwa moja hadi First League.
Kwenye Uwanja wa Black Rhino, Arusha, TMA itaikaribisha Copco wakati Biashara United itakuwa mwenyeji wa Cosmopolitan katika Uwanja wa Karume Musoma na kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam, Pan African itaikaribisha Stand United.
KenGold itakuwa mwenyeji wa Polisi Tanzania katika Uwanja wa Sokoine Mbeya na kwenye Uwanja wa Mabatini, Green Warriors watacheza na Ruvu Shooting.