Mavunde aibana kampuni kutimiza masharti ya mkataba

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde ameitaka Kampuni ya Xin Tai Mining Company Limited kutimiza masharti ya mkataba wa ubia wa uwekezaji  wa kutoa msaada wa kiufundi kwa kikundi cha wachimbaji wadogo cha Utulivu kilichopo eneo la Bululu, Wilayani Nyangh’wale Mkoani Geita. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).

Mavunde ameyasema hayo jana tarehe 27 Aprili 2024 katika Kijiji cha Bululu Wilayani Nyang’wale aliposhiriki mkutano wa utatuzi wa mgogoro uliopo baina ya baadhi ya wanakikundi cha Utulivu na Mwekezaji.

“Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ametupatia maelekezo mahsusi sisi Wizara ya Madini ya kuhakikisha tunashughulikia masuala ya changamoto za wachimbaji wadogo ili nao wanufaike na rasilimali za nchi yao.

“Kuanzia sasa tutaongeza umakini katika kuangalia mikataba hii ya msaada wa kifundi ili isiathiri malengo yaliyokusudiwa na sheria,” amesema.

Baada ya kusikiliza pande zote mbili za mgogoro huo, Mavunde alibaini uwepo wa Mkataba wa utoaji wa msaada wa kiufundi kwa Kikundi cha Utulivu, ambao umeeleza bayana masharti ambayo kampuni ya Xin Tai (Mwekezaji) anapaswa kutekeleza mara baada ya kusaini mkataba huo, .

Katika kutatua mgogoro huo, Mavunde alitoa sharti la kwanza kwa mwekezaji la kuhakikisha anafanya utafiti na kuchoronga eneo lote la leseni ya Kikundi cha Utulivu ili kubaini mashapo ambayo yatapelekea kuongeza uzalishaji na hivyo manufaa kwa wachimbaji wadogo kama mkataba ulivyomtaka.

Vilevile, *Waziri Mavunde* aliagiza kwamba Mwekezaji ahakikishe kama mkataba ulivyoeleza anapeleka mitambo na teknolojia ya kisasa kuwezesha uchimbaji katika eneo hilo, na kusisitiza kuwa hatarajii kuona teknolojia na zana duni ambazo hata wachimbaji wadogo wamekuwa wakizitumia.

Pia, Mavunde alimtaka mwekezaji kuhakikisha anaweka mitambo ya kuongeza thamani madini atakayoyachimba kama sharti la kimkataba lilivyoeleza ili kuwasaidia pia wachimbaji wadogo katika maeneo yanayowazunguka.

Aidha, Mavunde alionesha kutofurahishwa na namna utaratibu wa utoaji wa msaada wa kiufundi kwa wachimbaji wadogo unavyotekelezwa kwa sasa, na kuahidi kwamba ataenda kutoa maelekezo Bungeni tarehe 30 Aprili, 2024 wakati atakapowasilisha bajeti ya Wizara.

Awali, akimkaribisha Waziri kuzungumza katika mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella aliipongeza Wizara kwa namna inavyoshughulikia changamoto za wachimbaji wadogo na kuahidi kuwa Serikali ya Mkoa itaendelea kuunga mkono juhudi hizo za kuendeleza sekta ya madini nchini.

Akizungumza awali Mwenyekiti wa wachimbaji wa Wilaya Nyangh’wale, Jeremiah Misana ameipongeza serikali kwa zoezi la ufutaji Leseni na kuomba wachimbaji wadogo wapewe kipaumbele wakati wa zoezi la ugawaji wa maeneo.

Related Posts