Mawasiliano Pwani-Lindi yarejea baada ya barabara kukatika

Dar es Salaam. Sehemu ya barabara eneo la Kimanzichana mkoani Pwani, ilomeguka kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha, imekarabatiwa.

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, alitembelea eneo hilo lililopo Mkuranga katika njia kuu ya kuelekea mikoa ya kusini  leo Aprili 28, 2024.

Sehemu ya barabara eneo la Kimanzichana mkoani Pwani ilikatika kabla ya ukarabati. Picha na Mtandao

“Niwahakikishie Watanzania hamna haja ya kuwa na wasiwasi pamoja na mvua zinazoendelea kunyesha, ikitokea barabara imekatika, haitachukua nusu siku kwa namna ambavyo tumejipanga, tutakuwa tumesharudisha mawasiliano,” amesema Bashungwa.

Amesema Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), imejipanga kurejesha mawasiliano ya barabara zote na madaraja yanayoharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha nchini.

“Mkakati uliopo ndani ya Serikali ni kurudisha mawasiliano ya muda pindi inapotokea uharibifu wa miundombinu ya barabara na madaraja, huku ikisubiri kipindi cha kiangazi kianze na kufanya matengenezo ya kudumu katika maeneo yote yaliyopata athari,” amesema.

“Serikali inatambua mchango mkubwa wa barabara ya Mtwara-Lindi-Pwani-Dar es Salaam ni barabara ya kiuchumi na kimkakati ambayo inategemewa na wananchi, hivyo kupitia Tanroads wameanza kumtafuta mkandarasi atakayeanza kuijenga upya kuanzia Mtwara hadi Mingoyo na baadaye kuendelea kwa awamu mpaka Dar es Salaam,” amesema.

Ukarabati ukiendelea. Picha na Wizara ya Ujenzi

Bashungwa pia ametoa maelekezo kwa mameneja wa Tanroads mikoa yote kufanya ukaguzi wa madaraja na makaravati na kuondoa tope na takataka kwenye miundombinu hiyo, hususani madaraja.

Amemwelekeza Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Mhandisi Mohamed Besta, kusimamia kikamilifu makandarasi wote waliopewa kazi ya kurejesha miundombinu iliyoathiriwa na mvua kwa kufanya kazi kwa ufanisi na kumaliza ndani ya wakati.

Aidha, Waziri Bashungwa amelipongeza Jeshi la Polisi na wananchi kwa kutoa ushirikiano kwa watalaamu wa Tanroads na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) inapotokea changamoto yoyote kwenye barabara.

Related Posts