WAKATI Juma Mgunda akihusishwa na mipango ya kurudi kuifundisha Simba kutokana na kuondoka kwa Abdelhak Benchikha, kocha huyo maarufu kama ‘Guardiola Mnene’ amesema hata yeye anasikia tu kuhusu jambo hilo, lakini kama lipo kweli yeye atakuwa tayari kufanya kazi.
Simba inatarajiwa kutangaza kuachana rasmi na kocha Mbelgiji mwenye asili ya Algeria, Abdelhak Benchikha, ambaye taarifa zisizo rasmi zinadai ameomba kuondoka ili kwenda kumuuguza mkewe.
Akizungumzia na Mwanaspoti, Mgunda amesema yupo na timu ya Simba Queens na kesho ana mechi hivyo jioni ya leo atakuwa nayo tayari kwa mazoezi ya mwisho kabla ya kuwakabili JKT Queens.
“Mimi pia nasikia kama wewe, lakini lisemwalo lipo na kama lipo litakuja na litawekwa wazi hivyo acha tusubiri,” alisema na kuongeza;
“Mimi ni kocha na kazi yangu ni kufundisha ikiwa hivyo nitafanya kazi kama taaluma yangu inavyotaka nifanye.
“Nafurahi timu yangu inafanya vizuri, ushindi dhidi ya Yanga Princes umeongeza chachu ya ushindani, kesho nitakuwa uwanjani kuikabili JKT Queens, matumaini ni makubwa ya kuibuka na ushindi kwani timu yangu ipo vizuri na wachezaji wangu wana morali nzuri,” alisema.
Habari za ndani ya Simba zinaeleza kuwa kocha huyo ataungana na Suleiman Matola kwaajili ya kumalizia msimu huu wakiwa na mechi 9 kabla ya kumaliza msimu.
Wakati huo huo, Mgunda anawagawa viongozi kwani kuna ambao wanamuhitaji arudi huku wengine wakitoa pendekezo la kocha wa KMC, Mmarekani mzaliwa wa Somalia, Abdihamid Moalin ambaye ameiongoza timu hiyo kushika nafasi ya tano kwenye msimamo.
“Ndani ya Simba kuna mkanganyiko wapo wanaotaka Mgunda amalizie msimu wengine wakipinga hilo wakimtaja Moalin. Hivyo bado uamuzi haujafikiwa,” kilisema chanzo cha ndani ya klabu ya Simba.
Simba Queens watakuwa wenyeji wa mchezo dhidi ya JKT Queens na wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa na faida ya kuambulia pointi tatu na mabao matatu kutoka kwa wapinzani wao kutokana na kushindwa kufika uwanjani siku ya mchezo wao wa raundi ya kwanza msimu huu.