Mwanafunzi ajinyonga baada ya mpenzi wake kukamatwa

Mufindi. Mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya sekondari ya Mgololo iliyopo katika kata ya Makungu, Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa, Rahel Nyasi amekutwa amejinyonga katika mti wa shamba lililopo karibu na nyumba yao.

Akizungumza kwa njia ya simu leo April 28, 2024, Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mabaoni, Zephania Masanja, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo huku akisema mwanafunzi huyo anakadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 16 na 17.

Masanja amesema April 25, 2024 saa 2:00 asubuhi akiwa katika kitongoji cha Kidindi kilichopo kata ya Makungu, alipata taarifa kuwa kuna mtu amekutwa amejinyonga katika eneo hilo.

Amesema baada ya kupata taarifa hiyo, walifuatilia na kufika eneo la tukio na kuibaini kuwa aliyejinyonga ni mwanafunzi wa kike, aliyekuwa akisoma kidato cha pili katika shule ya sekondari ya Mgololo iliyopo katika kata hiyo.

“Tulipata taarifa ya mtu kujinyonga, hivyo tulienda hadi eneo la tukio na kufanya mawasiliano na Kituo cha Polisi Mgololo pamoja na daktari wa kituo cha afya ambapo walifanikiwa kuzungumza na wazazi na kufanya jitihada za kupima mwili. Ilibainika kuwa mwanafunzi huyo alijinyonga mwenyewe kwa kutumia mtandio mwekundu,” amefafanua mtendaji huyo

Mtendaji huyo amesema hadi sasa chanzo cha kujinyonga kwa mwanafunzi huyo bado haijafahamika, lakini Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha tukio hilo.

Amesema tukio hilo la kujinyonga ni la pili kutokea katika kijiji hicho ambapo mwaka 2023, mzee mmoja alifariki dunia kwa kujinyonga.

Masanja ameishauri  jamii kuacha tabia ya  kufanya maamuzi magumu pindi wanapokuwa na changamoto ambazo wanazipitia  badala yake wanatakiwa kushirikisha  watu wengine ikiwemo viongozi wa dini au  watu  wao wa karibu ili waweze kuwasaidia kutatua changamoto hizo.

“Niwasihi wananchi kuacha tabia ya kufanya maamuzi magumu ya kujitoa uhai kama mtu unapitia changamoto ni vema ushirikishe watu wa karibu hata viongozi wa dini ili waweze kushauriwa,” amesema Masanja.

Kwa upande wake, diwani wa kata hiyo, Felix Lwimbo ametoa wito kwa wazazi kuhakikisha wanakuwa karibu na watoto wao ili madhara kama hayo yasiwatokee.

“Mfano binti ambaye amejinyonga alikuwa anaishi na baba yake na mama yake alikuwa ameolewa sehemu nyingine baada ya wazazi hao kuachana, hivyo mtoto huyo alikosa malezi ya mama,” amesema diwani huyo.

Pia, amesema wazazi wanapaswa kuhakikisha wanalinda ndoa zao zisivunjike ili kuwapa malezi bora watoto wao.

Baba ataja sababu ya kujinyonga

Awali akizungumza tukio hilo, baba mzazi wa binti huyo, Onesmo Nyasi amesema mtoto wake amefikia uamuzi huo,  baada ya kijana anayedaiwa kuwa na uhusiano naye wa kimapenzi kukamatwa na polisi.

“Kabla halijatokea tukio la binti yangu kujinyonga ambapo ilikuwa April 24, 2024 alirudi nyumbani na kuniuliza swali kwamba nimemkamata kijana huyo kwa sababu gani? Lakini nilimjibu amekamatwa kwa ajili ya usalama wake,” amesimulia baba huyo.

Related Posts