Dar es Salaam. Benki ya NBC imepata tuzo ya mwezeshaji bora wa pamoja wa mikopo ya serikali kuu barani Afrika kwa mwaka 2023 katika Tuzo za Benki za EMEA.
Tuzo hiyo inalenga kutambua jitihada za benki ya NBC kama mwezeshaji mkuu wa mkopo wa Dola za Marekani 200 milioni kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo benki ya NMB ilikuwa mkopeshaji mwenza.
Fedha hizo zilielekezwa katika kuboresha huduma za kijamii na kuendeleza miundombinu muhimu Zanzibar, hatimaye kuboresha ubora wa maisha ya wakazi wake na kuwezesha ukuaji endelevu visiwani humo.
Tuzo hiyo inatajwa kuwa uthibitisho wa dhamira ya benki hiyo katika uwezeshaji wa miradi endelevu, ikionyesha kujitoa kwake katika kuimarisha jamii.
Kufuatia mafanikio hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi ameelekeza shukrani zake kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, wateja wa benki hiyo na wakopeshaji wenza kwa kuamini na kushirikiana nao.
Kwa mujibu wa Sabi, tuzo hiyo ni utambulisho siyo tu wa uzoefu wa benki katika shughuli za fedha, bali pia jukumu lake katika kuharakisha mabadiliko chanya na maendeleo katika jamii.
“Tuzo hii ni ushahidi wa uwezo wetu katika kurahisisha miamala ya fedha muhimu, pamoja na imani ambayo wadau wetu wametupa. Hii inatupa msukumo wa kuendelea kuboresha huduma zetu ili kuhamasisha maisha endelevu na kujibu mahitaji ya jamii zetu kwa weledi,” amesema.
Tuzo za Benki za EMEA nchini Afrika ni za heshima, zikitambua mafanikio ya kipekee katika sekta ya fedha na kuonyesha ubunifu na umahiri katika masoko ya mitaji barani Afrika. Mafanikio ya NBC katika tuzo hizo za heshima yanathibitisha dhamira yake ya kudumu kwa kuridhisha wateja na maendeleo ya jamii.
“Kwa zaidi ya miaka 50, Benki ya NBC inaendelea kuwa nguzo ya kuaminika katika sekta ya benki nchini Tanzania, ikiwasilisha wigo mpana wa bidhaa na huduma za kifedha ili kutimiza mahitaji mbalimbali ya wateja wake.
“Mafanikio haya katika tuzo za benki za EMEA ni ushahidi wa kujitolea kwa Benki ya NBC katika kujenga siku za usoni nzuri kwa wote,” ameongeza Sabi.