NCAA kutetea nafasi yake tuzo ya kivutio bora cha utalii Afrika

Arusha. Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), imezindua kampeni yake ya kuipigia kura mamlaka hiyo kutetea nafasi yake ya kuwa kivutio bora cha utalii barani Afrika, kwa mwaka 2024 zinazotolewa na mtandao wa World Travel Awards.

Oktoba 15, 2023, Ngorongoro ilinyakua tuzo hiyo baada ya kushinda vivutio vingine vya utalii barani Afrika ikiwemo Table Mountain, Hartbeespoort Aerial Cableway, V &A Waterfront, Ruben Island vya Afrika Kusini na Okavango Delta cha Botswana.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili Aprili 28, 2024 jijini Arusha, Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa mamlaka hiyo, Victoria Shayo amesema NCAA, mwaka huu inatarajia kushindana na vivutio vingine vinane.

Amesema vivutio hivyo vipo katika nchi tano za Afrika ambazo ni Afrika Kusini, Botswana, Misri pamoja na Malawi.

Amesema Aprili 4, 2024, mtandao huo ulitangaza orodha ya makundi mbalimbali kwa ajili ya kuwania tuzo mbalimbali ambazo hutolewa na mtandao huo na kushindanishwa katika ngazi ya mabara ambapo kwa mwaka huu, mamlaka hiyo imeteuliwa kuwania tuzo hiyo tena.

“Ushindi wa mwaka jana haukuwa kwa mamlaka pekee bali kwa wadau wa utalii, uhifadhi na Tanzania kwa ujumla na leo Aprili 28, NCAA inazindua ramsi kampeni ya upigaji kura kwa mwaka huu ambayo itaenda kwa kaulimbiu isemayo “You Vote We Win” na dirisha la upigaji kura lilifunguliwa tangu Aprili 2, mwaka huu na litaendelea hadi Septemba 8, 2024,” amesema.

Akizungumzia hatua ya mamlaka hiyo kufunga kwa muda baadhi ya barabara zake kutokana na kuharibiwa na mvua, amesema wana mikakati ya kuimarisha miundombinu ikiwemo ya barabara ili kupunguza adha ya kurekebisha kila mwaka kipindi cha mvua ikiwemo kuweka tabaka gumu katika barabara kuu ya mamlaka hiyo.

Naye Kamishna wa uhifadhi msaidizi mwandamizi anayeshughulikia huduma za utalii katika mamlaka hiyo, Mariam Kobelo ametoa wito kwa Watanzania, wadau wa utalii wa ndani na nje ya nchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura.

“Ukiangalia shughuli ya upigaji kura kwa njia ya mtandao haichukui hata dakika mbili, niwaombe sana Watanzania na wadau wengine wa utalii kutoka ndani na nje ya nchi kupiga kura kwa wingi, na nyie wanahabari tunaomba msaidie kuwahamaisha wadau kupiga kura ili tuchukue ushindi na mwaka huu na kurudi na kombe,” amesema.

Related Posts