Serikali kununua helikopta maalumu kutafiti madini

Geita. Waziri wa Madini, Antony Mavunde amesema Serikali kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), kwa mwaka ujao wa fedha inakusudia kununua helikopta itakayofungwa vifaa maalumu vyenye uwezo wa kwenda chini umbali wa kilomita moja na kutafiti kwa kina kiwango cha madini kilichopo ardhini.

Pia, Serikali inalenga kujenga maabara kubwa na ya kisasa mkoani Dodoma, ili wachimbaji waweze kupima sampuli za udongo kwa gharama nafuu na kuokoa fedha zao wanazotumia sasa kwenye maabara binafsi ambazo zinatoza gharama kubwa.

Akizungumza jana April 27, 2024 wakati akitatua mgogoro baina ya wanakikundi cha uchimbaji madini cha Utulivu na wachimbaji wenye mashimo (duara) kwenye eneo lililopo Bululu wilayani Nyang’hwale mkoani Geita, Mavunde amesema lengo ni kuwaongoza wachimbaji kujua sehemu yenye madini ili mitaji yao isipotee.

Waziri Mavunde amesema  lengo la wizara hiyo ni ifikapo mwaka 2030, eneo lililofanyiwa utafiti wa kina liongezeke kutoka asilimia 16 zilizopo sasa hadi kufikia asilimia 50, jambo ambalo litasaidia wale wanaoomba leseni kupewa maeneo yenye uhakika na sio ya kubahatisha.

“Mafanikio haya mnayoyaona yanatokana na utafiti uliofanywa kwa asilimia 16 tu na hii ndiyo imefanya sekta ya madini iongoze katika kuiingizia nchi fedha za kigeni. Mauzo ya bidhaa nje ya nchi mwaka uliopita yalikuwa Dola za Marekani 3.1 milioni, sawa na Sh7 trilioni na yalitoka kwenye sekta ya madini”

“Maduhuli Serikali iliyokusanya ni Sh678 bilioni, mapato ya kodi ya ndani tumechangia Sh2.1 trilioni sawa na asilimia 15 ya mapato yote ya ndani na hii ndio imetufanya tukae tujiulize kama sehemu hii ndogo ya utafiti imeleta mafanikio haya, je, tukienda mara tatu zaidi nchi itakuwa vipi?” amesema Mavunde.

Ameongeza: “Tukifika asilimia 50 ya utafiti wa kina tutaondoa migogoro kati ya wachimbaji wakubwa na wadogo, utajiri wa mchimbaji yeyote ni taarifa, usipokuwa na taarifa, leseni uliyonayo ni sawasawa na gazeti na huwezi kulitumia kama dhamana ya mkopo.’’

Akizungumzia mgogoro uliodumu kwa miezi mitatu baina ya wachimbaji hao kufuatia kikundi cha Utulivu kutoa maeneo ya uchimbaji kwa mwekezaji wa nje, Waziri Mavunde ametoa siku saba kwa ofisa madini mkoa wa kimadini Mbogwe kuzungumza na baadhi ya wanakikundi wanaopinga uwekezaji na kufikia mwafaka.

Pia, amemtaka ofisa madini huyo kuwataka wawekezaji waliopewa eneo hilo kufanya utafiti wa kina kwenye eneo lote walilopewa kama mkataba wao unavyosema badala ya kuchukua eneo la wachimbaji wadogo na kuwa utafiti huo ukifanyika utaongeza uzalishaji.

Kuhusu wenye maduara kwenye eneo hilo, Mavunde ametaka wenye mawe yaliyozalishwa na wenye maduara kupewa kwa kuwa ni haki yao ya msingi, pamoja na kuwataka wanakikundi wa Utulivu kukaa na wale waliokataa kuchukua fedha wafikie mwafaka na kulipa gharama walizotumia kuchimba mashimo hayo.

Akizungumza na wachimbaji hao wa Bululu, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela amesema kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita, leseni zaidi ya 2000 zimetolewa kwa wachimbaji wadogo wa mkoa huo.

Amesema ukuaji wa uchumi na maisha mazuri ya wananchi wa mkoa huo, vinatokana na shughuli za uchimbaji madini na kuwataka kutoendekeza migogoro kwa kuwa inawacheleweshea kupata maendeleo.

Awali, wakizungumza na waziri, katibu wa kikundi cha Utulivu, Solomon Mabati amesema kikundi hicho kinachoundwa na vikundi vidogovidogo 13 kwa pamoja waliamua kutoa eneno lao kwa mwekezaji kutokana na uchimbaji wa moko kuhatarisha maisha lakini pia eneo la mwamba kuwa mbali, hivyo kutofikiwa kwa urahisi.

Mashamba Bulugu, mmoja wa waliokuwa na mashimo kwenye eneo hilo,  amesema walikaribishwa na viongozi wa Utulivu kuchimba na kuweka nguvu zao kwa kipindi cha miaka minne, lakini baada ya kufikia mwamba ndipo wametakiwa kuondoka kabla ya kurudisha gharama walizotumia.

Related Posts