Simba yaifuata Namungo bila Benchikha

KIKOSI cha Simba kimewasili kutoka Zanzibar ambako kimetwaa taji la sita la Muungano na kuunganisha moja kwa moja kuifuata Namungo tayari kwa mchezo wa ligi utakaochezwa Jumanne.

Lakini pia gazeti hili limepenyezewa kuwa kocha wa fitness (utimamu) pia hayupo kwenye msafara wa kikosi cha timu hiyo ikielezwa kuwa anaondoka sambamba na Benchikha ambaye alikuja naye.

Simba imeanza moja kwa moja safari ya kwenda Lindi, bila ya kocha wao mkuu, Benchikha ambaye inaelezwa kuwa tayari amemalizana na uongozi baada ya makubaliano ya pande mbili.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba, kimeliambia Mwanaspoti kuwa safari ya kwenda Lindi inaongozwa na kocha msaidizi wa timu hiyo Selemani Matola ambaye ndiye atakiongoza kikosi hicho kwenye mchezo wa mzunguko wa pili dhidi ya wenyeji Namungo.

Ipo hivi; Mara baada ya timu kufika bandarini kocha alipanda gari ndogo kwenda hotelini ambako anaishi huku timu ikipanda basi tayari kwa safari kuifuata Namungo.

“Timu inaondoka na kocha msaidizi Matola, safari inaunganishwa hakuna kwenda kambini wala wachezaji kuruhusiwa kwenda makwao baada ya kutua bandarini tumepanda basi moja kwa moja kuanza safari ya kwenda Lindi,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

“Kocha mkuu hatakuwa sehemu ya mchezo huo kwani tayari amewaaga wachezaji na benchi la ufundi mara baada ya kutwaa Kombe la Muungano, nafikiri sasa timu itakuwa chini ya Matola,” kilisema chanzo hicho.

Simba itashuka dimbani kumenyana na Namungo iliyo chini ya kocha, Mwinyi Zahera ikiwa na kumbukumbu ya kuambulia sare ya bao 1-1 kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza kwa Mkapa.

Related Posts