Simba yamrejesha Juma Mgunda | Mwanaspoti

Hatimaye Simba imerejesha kocha mzoefu, Juma Mgunda kwenye kikosi hicho muda mchache baada ya Abdelhack Benchikha na wasaidizi wake kutimka.

Tetesi zilianza kuzagaa wiki nzima kuwa Benchikha anaondoka kwenye kikosi hicho na muda mchache uliopita, Simba imetoa taarifa ya kuachana naye na sasa timu hiyo itakuwa chini na Mgunda na Selemani Matola.

Taarifa iliyotolewa na Simba, inasema uongozi wa timu hiyo umeachana na Benchikha baada ya kocha huyo kuomba kuvunja mkataba kutokana na matatizo ya kifamilia yanayomkabili.

“Uongozi wa klabu ya Simba umefikia makubaliano ya pande mbili kuachana na kocha mkuu Abdelhak Benchikha pamoja na wasaidizi wake wawili, Mwalimu Benchikha ameomba kuvunja mkataba wake kutokana na matatizo ya kifamilia yanayomkabili.

“Wakati huohuo, uongozi umemteua Mwalimu Juma Mgunda kukiongoza kikosi hicho akisaidiwa na Selemani Matola hadi hapo Bodi ya Ukurugenzi itakavyoamua vinginevyo,” ilisema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo inasema Mgunda ambaye aliwahi kuifundisha Coastal Union na Simba kwa vipindi tofauti, ataanza kazi kwenye kikosi hicho kwenye mchezo wa kesho dhidi ya Namungo.

Related Posts