Simulizi ya mwanafunzi mchoraji mwenye uoni hafifu

Bukoba. “Nilianza kuchora picha ya chupa ya maji, baadaye nilichora picha ya baba yangu mzazi, kwa sasa nimechora picha ya mbunge wangu, na picha hii ni zawadi kwake. Natamani kusoma chuo  Korea na China ili kuendeleza kipaji changu na kuinua familia yangu yenye uhitaji mkubwa.”

Hayo ni maneno ya Julieth Richard (19), msichana mwenye uoni hafifu, mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya sekondari Bukoba, mwenye kipaji cha uchoraji licha ya changamoto yake ya kutumia jicho moja.

Safari yake ya kielimu ilianzia shule ya msingi Mafumbo, kata ya Kashai, Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera ambapo licha ya kujifunza masomo ya kawaida, alikuwa akijifunza pia kuchora, kipaji ambacho amezaliwa nacho.

Msichana huyo amepata umaarufu katika kisiwa cha Msira kilichopo Ziwa Victoria baada ya kuchora picha ikimuonyesha mbunge wa jimbo la Bukoba mjini (CCM) ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje (Ushirikiano wa Afrika Mashariki), Stephen Byabato.

Julieth alizaliwa katika Mtaa wa Msira ambao ni miongoni mwa mitaa mitano inayounda kata ya Miembeni iliyopo manispaa ya Bukoba. Tofauti ya mtaa huo na mingine ni kwamba ndiyo kisiwa pekee kwenye jimbo la Bukoba Mjini.

Kisiwa hicho ni makazi ya watu 317 ikiwa wanaume ni 184 na wanawake 133, kina huduma za kijamii kama sehemu nyingine na jamii inayoishi ndani ya kisiwa hicho ni wavuvi wa samaki na dagaa kwenye ziwa hilo.

Akizungumza na Mwananchi kwenye mahojiano maalumu leo Aprili 28, 2024, Julieth amesimulia kwamba kipaji chake kiligundulika akiwa darasa la saba katika shule ya msingi Mafumbo mwaka 2020 baada ya kufikiria kitu anachoweza kufanya kuwasaidia wazazi wake na ndugu zake wengine saba ambao wanakabiliwa na changamoto za kiuchumi.

Amesema alipenda uchoraji baada ya kukutana na rafiki yake shuleni akiwa mtaalamu wa fani hiyo, akavutiwa na kipaji chake. Anasema alianza kujifunza kwa bidii na hatimaye akafanikiwa kujua na hadi sasa amechora picha tatu zilizompa umaarufu.

Msichana huyo anasema ana uwezo wa kutumia muda wa kuanzia saa tatu hadi siku tatu kuchora picha ya mtu au kitu.

Alivyochora picha ya mbunge

Julieth ameeleza kwamba sababu ya kuchora picha ya mbunge wake, Byabato ni kutokana na kuvutiwa na uwajibikaji wake katika majukumu ya kibunge kwenye jimbo hilo hasa katika kusaidia Serikali kuleta maendeleo kwenye kisiwa cha Msira alipozaliwa.

Amesema kisiwa hicho ni kati ya maeneo machache yaliyokuwa na changamoto mbalimbali na viongozi wengi waliopita kwenye uongozi, hawakuweka kipaumbele kwa maana changamoto zilikuwa nyingi ikiwemo ukosefu wa miundombinu ya usafiri kwa wanafunzi kutoka kisiwani Msira hadi shule zilipo.

Hata hivyo, amesema changamoto hiyo imetatuliwa kwa kutengenezewa boti ya MV Byabato kwa gharama inayotumiwa na wananchi wa eneo hilo ambapo wanafunzi wanapanda bure kwenda shule na kurudi nyumbani kila siku.

“Kikubwa zaidi kilichonifanya nimchore mbunge wetu ni jinsi anavyowajibika katika kazi alizopangiwa na Taifa kama mbunge na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje. Tulikuwa hatuna usafiri wa kutupeleka shule, katupatia tayari, tulikuwa hatuna choo kizuri kwenye mtaa wetu, sasa hivi tumefanikiwa kukipata na mambo mengine mengi. Nampongeza sana ndiyo maana nimemchora,” amesema Julieth.

Julieth amesema watoto wa kike mara nyingi wanawachukulia kama watu dhaifu na hawapati uwezeshaji pale wanapoonekana wanakipaji fulani, anaamini Tanzania ina vipaji vingi vya watoto wa kike wenye uwezo tofauti kama mpira, uchoraji na vingine vingi vinavyoweza kuingizia pato na kukuza uchumi wa nchi.

Hata hivyo, amesema hawawezeshwi inavyotakiwa, hivyo anatamani kuona dhana hiyo inafutika kwenye jamii na Taifa kwa ujumla kwani dunia imebadilika na nchi nyingi ikiwemo Tanzania wanawake wameonyesha kuwajibika ipasavyo katika sehemu mbalimbali.

Mama mzazi wa Julieth,  Koncharatha Bazil (49) amesema mwanawe alinza kuona kipaji chake tangu akiwa mdogo kwa kuwa alipenda kuchora vitu mbalimbali kama samaki, mitumbwi na miti na mwaka 2020 alizungumza naye akamuambia anapenda kuchora.

Amesema anahisi anaweza kupiga hatua kielimu na kimaisha kupitia kipaji hicho licha ya kuwa mwanzoni hakumwelewa mwanaye, lakini alikuja kuamini kuwa kweli kipaji kimekua baada ya kumchora baba yake.

Koncharatha amesema alikuwa anapata wasiwasi kuhusu kipaji cha mwanawe kuwa kitafifia baada ya familia yao kupitia wakati mgumu kwa sababu baba yake alipata changamoto za kiafya kutokana na kazi zake za uvuvi alizokuwa kizifanya ndani ya Ziwa Victoria kusimama baada ya kuchomwa mfupa wa samaki mkononi na kumsababishia matatizo ya kiafya.

“Julieth ni mtoto wangu wa tano, anapenda uchoraji lakini sina hela na vifaa hana, naogopa sana kupoteza kipaji chake maana sina uwezo, nina watoto saba, wa kike watano, wa kiume wawili, sina uwezo wa kuwaendeleza kielimu,” amesema mama huyo.

Mama huyo amesimulia kwamba tatizo la Julieth kutoona kutoona vizuri lilianza akiwa na umri wa miaka miwili na nusu, alipougua homa kali iliyosababisha akalazwa hosipitali ya mkoa Bukoba kwa mwezi mmoja akisumbuliwa na kuishiwa damu mara kwa mara.

Amesema alianza kuona dalili zikijitokeza baada ya mwanaye kuvimba kwenye maeneo alipokuwa anachomwa sindano akiwa hospitalini kwa sababu maumivu yalikuwa na tabia ya kuhama hadi jicho likaanza kuonyesha dalili za kuwa jekundu, akamrudisha hospitalini aone kama mwanawe atatibiwa lakini ilishindikana.

Alianza kushauriwa na watu kuwa amepata madhara ya dawa kutokana na hali ya uchumi, hakuwa na uwezo tena wa kumpeleka  hospitali kubwa za kibingwa, hivyo ikasababisha mwanae kupoteza  uoni wa jicho moja la kulia.

Dafroza Pachal, mkazi  wa Mtaa wa Msira ameeleza anavyoshangazwa na kipaji cha huyo mtoto huyo kwa maana jamii imezoea kuona watoto wa kiume ndiyo wenye uwezo na  kuchoraji lakini kwa huyo wa kike imewashangaza.

“Huyu mtoto ni tunu ya taifa, tunaomba viongozi wamuendeleze, ana uwezo mkubwa wa kuchora, nina watoto wengi na huu mtaa una watoto wengi lakini sasa huyu ndio kiboko yao,” amesema.

Mwenyekiti wa mtaa huo, Jacob Soud amesema amefanya kazi hiyo ya uongozi kwa kipindi kirefu na ameona watoto wengi wenye vipaji lakini msichana huyo ni ana maajabu Mungu, amewaomba viongozi wajitokeze kuendeleza kipaji chake.

Byabato alipata fursa ya kukutana na msichana huyo alipotembelea kisiwa cha Msira na kufanya mkutano wa hadhara na kusikiliza kero za wananchi ambapo alikabidhiwa picha yake na kuahidi kumsaidia kila atakapokuwa anapata nafasi.

Byabato ameendesha harambe ya kumchangia binti huyo mwenye kipaji cha kuchora na kufanikiwa kupata fedha tasilimu Sh200,000 zilizomwezesha kununua vifaa vya kufanya shughuli za uchoraji ambavyo vitamsaidia Julieth kuchora na kupata matumizi ya shuleni.

Related Posts