Wafugaji wataka bima ya mifugo

Dar es Salaam. Wafugaji wameomba kuwe na bima ya mifugo iwapo watakufa au kupata ajali, ambayo itafungua fursa zaidi za soko la ajira katika mnyororo wa thamani.

Akizungumza leo Jumapili Aprili 28, 2024 katika hafla ya Siku ya Uwekezaji ya Benki ya CRDB, Mwenyekiti wa Wafugaji Tanzania, Mrida Marocha amesema wanahitaji bima ya mifugo ambayo itawahakikishia usalama wa mifugo yao.

“Mifugo inathamani ambayo inaingiza pesa nyingi lakini haina bima kama ilivyo kwenye magari, CRDB wakae wawafikirie wafugaji kuwawekea bima,” amesema Marocha.

Amesema ufugaji wa sasa ni tofauti na zamani walipokuwa wanahama-hama na kuwa vigumu kukopesheka katika benki kwa kuhofia kupoteza pesa zao.

Amesema kwa sasa wamesajili wafugaji zaidi ya 12,000 kutoka katika kata, wilaya, mkoa na Taifa kwa ujumla na wanatarajia baada ya miaka mitatu wawe wamesajili wanachama milioni nne.

Marocha pia ameomba kuwe na uwezeshwaji wa viwanda vya usindikaji ili kurahisisha biashara ya mifugo.

“Endapo wenye viwanda vya usindikaji watasaidiwa, wafugaji watapata pesa zao kwa wakati kuliko kuambiwa waache mifugo kwanza kisha warudi kufuata pesa baada ya muda, hii inarudisha nyuma sekta ya mifugo,” amesema.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amewataka wataalamu wa fedha na uchumi nchini kuwasaidia wavuvi na wafugaji kwa kutumia fursa zilizopo katika sekta hiyo, hususani wavuvi wa dagaa katika maziwa Tanganyika na Victoria.

“Biashara za nyama na dagaa zina thamani kubwa kwa sasa, wananchi wanatakiwa kuwekeza katika maeneo hayo kwani dagaa wa Kigoma wanauzwa kwa kiroba Sh60,000, hivyo tunatakiwa kusaidia watu wetu,” amesema.

Amesema vitumike vifungashio maalumu kwa ajili ya kuthamini dagaa hao na si kuwaweka kwenye viroba.

Waziri ameeleza nchi jirani wanatumia fursa ya kununua kwa viroba na kuuza kwenye mataifa mengine.

Amesema yanahitajika mabadiliko katika sekta za uvuvi na mifugo kwa kutumia fursa zilizopo kuchechemua uchumi.

Mmoja wa waanzilishi wa Benki ya CRDB Kanda ya Magharibi, Gosbert Ndegumisa amesema thamani iliyopo kwenye mifugo ni kubwa kwa kuwa na uhakika wa uuzaji wake ambao unaingiza hadi Sh200 milioni.

“Wafugaji ni matajiri na wana uhakika wa maisha baada ya kuuza ng’ombe, hivyo kuna haja kubwa ya kuangalia ni namna gani wanawezeshwa kwenye bima ya mifugo,” amesema.

Related Posts