Wataka maandamano ya Chadema vijijini

Sengerema. Wananchi wa Sengerema mkoani Mwanza wamewashauri viongozi wa Chadema kushusha maandamano ya amani hadi ngazi ya vijiji, ili kuwasaidia wananchi wa maeneo hayo kupata uelewa wa pamoja kuhusu malengo ya maandamano hayo.

Wametoa ushauri huo leo Aprili 28, 2024 kufuatia maandamano ya Chadema yaliyofanyika jana Aprili 27, wilayani humo na  na kuongozwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe

Wananchi hao wamesema maeneo ya mijini, watu wengi wana uelewa mkubwa wa mambo kuhusu mustakabali wa nchi yao lakini vijijini bado watu wengi hawana mwamko wowote, hivyo wakishusha chini maandamano hayo itawasaidia wananchi kupata mwamko wa mabadiliko.

Mkazi wa Sengerema, Julius Atanasi amewataka Chadema kupokea ushauri wao kama wananchi kuhusu kwenda vijijini kufanya maandamano hayo ya amani ambayo yamekuwa na matokeo chanya.

“Chadema wanatakiwa kujikita vijijini kutoa elimu kwa wananchi kuhusu maandamano ya amani wanayoyafanywa sehemu mbalimbali nchini,” amesema Atanasi.

Kwa upande wake, Jastine Wiliam, mkazi wa kijiji cha Kanyali, jimbo la Buchosa ambaye ameshiriki maandamano hayo, amesema Chadema ikijikita vijijini na kuondoka mijini, itawaamsha wananchi walioko vijijini kuhusu mabadiliko yanayopiganiwa na chama hicho.

Hata hivyo, Kazimili Jonathan, mkazi wa kijiji cha Nyamatongo, wilayani humo amesema kufuatia maandamano yanayofanyika mjini, ambako watu wana uelewa zaidi, Chadema inatakiwa kubadilisha mfumo, hivyo kujikita vijijini zaidi itaisaidia wananchi kuelewa sera za mabadiliko za chama hicho.

“Vijijini kuna watu wengi ambao wanahitaji kupata nguvu ya mabadiliko, hivyo lazima tujikite huku tukafanye maandamano ya amani na kuwaeleza dhana nzima ya mabadiliko,” amesema Jonathan.

April 27, 2024, Chadema wamefanya maandamano ya amani wilayani Sengerema yaliyoongozwa na Mbowe ambapo baada ya maandamano hayo , alifanya mkutano wa hadhara na kuzungumuza na wananchi kwenye viwanja vya stendi ya zamani mjini hapa.

Wakati akiwahutubia wananchi wa Sengerema, Mbowe amesema mpango wa chama hicho ni kwenda ngazi ya vitongoji, mitaa, vijiji na kata kupeleka ujumbe wa maandamano ya amani.

“Awamu ya kwanza ilikuwa ya kwenda kwenye majiji na miji yote pamoja na mikoa, sasa tunakuja na ngazi ya vitongoji, mitaa, kata na wilayani zote kufanya maandamano ya amani,” amesema Mbowe.

Katika hatua nyingine, Mbowe amesema chama hicho hakijakubaliana na Serikali katika mfumo  wa uchaguzi ndani ya nchi, akidai ni mfumo kandamizi ambao hauwezi kutoa haki kwa vyama vya siasa kwenye uchaguzi.

 Amesisitiza umuhimu wa kuwa na Katiba mpya ili kubadili mfumo huo na  haki itendeke.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bawacha Taifa, John Pambalu amesema mateso yanapozidi kwa Watanzania ya ugumu wa maisha, ndivyo ukombozi wao unavyokaribia, hivyo Watanzania wanatakiwa kuchukuwa hatua na uamuzi kwenye uchaguzi mkuu wa serikali za mitaa.

Pambalu amedai kuwa maisha ya Watanzania yamekuwa magumu baada ya baadhi ya vitu kupanda bei akitolea mifano mtungi mdogo wa gesi awali ulikuwa ikiuzwa Sh17,000 kwa sasa unauzwa Sh25,000, sukari ilikuwa inauzwa Sh2,500, kwa sasa ni Sh4,000, hivyo uamuzi wa kweli unatakiwa kufanywa na wananchi ili wakombolewe.

Related Posts