7 wafa Ulanga, mbunge alia kutelekezwa na mawaziri, Tanroad

Watoto saba wamepoteza maisha na zaidi ya kaya 70 kukosa makazi Wilaya ya Ulanga Mkoani Morogoro kutokana na athari za mafuriko yaliyotokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha wilayani Humo na nchini kwa ujumla. Anaripoti Mwandishi Wetu… (endelea).

Mbunge wa Ulanga, Salim Hasham amebainisha hayo jana Jumapili wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Morogoro juu ya athari za mafuriko yaliyowakumba wakazi wa jimbo lake na kusisitiza kuwa hali ni mbaya kwa sasa na waathilika wanahitaji msaada wa dharula.

Mbunge ametaja athari nyingine ni pamoja na wananchi kupoteza heka 5,000 za mazao yaliyokuwa shambani na kuwaacha wananchi wengi wakiwa hawana chakula hali iliyomlazimu kupaza sauti kwa Seikali na wadau wengine kuangalia namna ya kuwanusuru waathilika hao wa mafuriko.

Akizungumzia hali ya miundombinu ya barabara Mbunge huyo Ulanga amewaambia waandishi wa habari kuwa  kwa sasa mawasiliano ya barabara ya Lupiro – Mahenge yamekatika na kusababisha adha kubwa ya usafiri kwa kuwa hakuna magari yanayoweza kuingia na kutoka katika mji wa Mahenge ambao ni makao makuu ya wilaya.

Amesema kulingana na adha hiyo gharama ya maisha imepanda maradufu kwani kutokana na wafanyabiashara kufikisha bidhaa hiyo kwa ugumu zaidi, huku akibainisha kuwa kwa sasa kilo moja ya chumvi iliyokuwa inauzwa Sh 500 sasa inauzwa Sh 2,000, sukari imepanda na kufikia Sh 7,000, wakati unga ukiuzwa kwa zaidi ya Sh 3,200, gharama ambayo wananchi walio wengi hawawezi kuimudu.

Salim amesema gharama za maisha zimepanda zaidi kutokana na miundombinu ya barabara kuharibika na kusababisha magari kushindwa kufanya safari za kuingia na kutoka MAkao makuu ya wilaya ya Ulanga, huku akieleza kusikitishwa na ukimya wa Wakala wa Barabara (Tanroad) licha ya kufikishiwa changamoto iliyopo kwa zaidi ya miezi minne sasa.

“Hatuwezi kuilaumu Serikali, kwa uzembe unaofanywa na watendaji waliopewa mamlaka ya kufanya hizo shughuli na kushindwa kutimiza wajibu wao kwa kisingizio cha mvua” alisema.

Aidha, pia amekanusha uvumi kuwa Tanroads walimpiga faini, baada ya yeye binafsi kuamua kurekebisha baadhi ya maeneo yaliyoharibika akisisitiza kuwa taarifa hizo hazina ukweli wowote bali zinapotoshwa na baadhi ya watu wasio na mapenzi mema kwa wana Ulanga wanaotamani kuona wananchi wanaendelea kutaabika.

Katika Hatua nyingine, Mbunge huyo alisema licha ya mvua kuendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali lakini kinachosikitisha zaidi ni kuona hakuna hata kiongozi mkubwa aliyefika kuwafariji wananchi wa Ulanga hali inayowafanya wananchi kujihisi kuwa wametengwa na Serikali yao na kujiona kuwa siyo sehemu ya Wanzania.

“Tunaamini kuwa hali ya mvua inaendelea nchi nzima na inawezekana tusipate msaada wa haraka kutokana na hali inayoendelea, lakini hatuhitaji mje mtusaidie lakini Serikali tunahitaji tupate faraja wananchi wa jimbo la ulanga wanahitahi faraja.

‘Sasa taarifa zinaenda kwa mawaziri, zinafika kila sehemu tunaona jinsi ambavyo mawaziri wanatembea kila sehemu kwenda kuangalia adha inayowakuta wananchi katika maeneo yao, lakini jimbo la Ulanga limekuwa kama siyo Tanzania  inafika wakati wananchi wa Ulanga Wananiuliza kwamba labda sisi siyo Watanzania labda sisi Rais wetu siyo Mama Samia Suluhu Hassan?” alisema.

Alisema amelazimika kuzungumza na vyombo vya habari ili Rais Dk. Samia licha ya kuwa kipenzi cha wananchi wote lakini ajue ni aina gani ya watendaji anaowaajiri namna wanavyomuangusha katika kuwatetea wananchi wanyonge

Related Posts