Barabara hazitajengwa pembeni mwa reli ya SGR

Dodoma. Serikali imesema haitajenga barabara za lami kwa matumizi ya kawaida pembezoni mwa Reli ya Kisasa (SGR), kwa sababu Sheria ya Reli ya Mwaka 2017 hairuhusu kufanya hivyo.

Hayo yameelezwa bungeni leo Jumatatu Aprili 29, 2024 na Naibu Waziri wa Ujenzi, Geofrey Kasekenya alipojibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Janeth Massaburi.

Mbunge huyo ametaka kufahamu iwapo Serikali ina mpango wa dharura wa kujenga barabara kwa kiwango cha lami pembezoni mwa Reli ya SGR wakati ujenzi unaendelea.

Kasekenya amesema kwa mujibu wa Sheria ya Reli Na. 10 ya mwaka 2017, hifadhi ya reli ni mita 30 kutoka katikati ya reli kila upande. 

“Katika eneo hili hairuhusiwi kujenga barabara kwa matumizi ya kawaida. Hivyo, haitawezekana kujenga barabara ya lami pembezoni mwa SGR,” amesema.

Katika siku za karibuni wakati ujenzi SGR unaendelea, watumiaji wengi wa vyombo vya moto wamekuwa wanatumia njia za vumbi za mkandarasi pembeni mwa reli hiyo, kama njia mbadala za kukwepa foleni kwenye Barabara ya Nyerere jijini Dar es Salaam.

Katika maswali ya nyongeza ya Massaburi yalihoji barabara za msunguko na mitaro ili kupokea maji ya mvua jijini humo, Kasekenya amesema ujenzi wa barabara za mzunguko kwa Mkoa wa Dar es Salaam uko kwenye mpango kabambe na kwa sasa imeshampa kazi mhandisi mshauri kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu.

Kuhusu ujenzi wa mitaro, amesema  kumekuwapo na makubaliano kati ya Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) kuhakikisha wanatoa kipaumbele cha ujenzi wa mifereji kwa barabara wanazojenga.

Related Posts