BASSFU YATUA MKUNAZISAMAKI KUSIKILIZA WANANCHI

Na Rahma Khamis Maelezo 29/4/2024.

Wananchi wa Shehia ya Kisauni na Muungani wameliomba Baraza la Sanaa, Sensa ya Filamu na Utamaduni (BASFU) kuichunguza kwa makini Baa ya Oxygen iliopo Mkunazisamaki ili kuondosha matatizo yanayojitokeza katika shehia hizo.

Wakitoa malalamiko katika mkutano, ulioandaliwa na BASFU kwa ajili ya kusikiliza malalamiko ya wananchi wamesema Baa hiyo inapigwa muziki kwa sauti kubwa jambo ambalo linaathiri jamii ikiwemo wagonjwa waliopo majumbani.

Aidha wamesema kuwa uwepo wa Baa hiyo pia kunasababisha mporomoko wa maadili kwani baadhi ya vijana wanajishirikisha na vitendo vya uuzaji na utumiaji wa dawa za kulevya pamoja na bangi.

Pia wameliomba Baraza hilo, kufuatilia kwa makini vitendo vinavyofanyika katika baa hiyo ikiwemo kuhatarisha amani kwa wakaazi wa maeneo hayo.

“Kweli vitendo vinavyofanyika katika Baa hiyo sio vizuri hata kidogo unakuta watu wanalewa na kupiga watu mitaani na kikubwa zaidi hivi karibuni kama tunavyojuwa ilikuwa ni mwezi mtukufu wa Ramadhani, watu walikuwa wanapenya mlangoni na chupa na huku wakila mchana kweupe.” alisema Wakaazi hao.

Sambamba na hayo wamesema kuwa Baa hiyo inasababisha wanawake na watoto kufanyiwa vitendo viovu ikiwemo kubakwa na kupigwa jambo ambalo linawaathiri na kuwatia hofu ya kutembea hasa wakati wa usiku.

Hata hivyo wameiomba Taasisi inayoshughulikia masuala ya vinywaji na vileo kufika katika eneo hilo ili kuweza kuona matatizo yaliopo na kuyapatia ufumbuzi wa haraka ikiwemo kuifungia Baa hiyo.

Kwa upande wake Mrajis wa Baraza hilo Juma Chuom Juma amesema tayari wameshapiga marufuku kufanya shughuli zote za Sanaa lakini uongozi wa Baa hiyo umeendelea kukaidi agizo hilo.

Hivyo amewaomba wananchi kuwa wastahamilivu kwani Serikali inalifahamu tatizo hilo na inafanya kila jitihada ili kuondosha athari kwa wananchi.

“Serikali kupitia Wizara yetu chini ya BASSFU tumechukuwa hatua ya kuifungia mara baada ya kupokea malalamiko yenu lakini ndugu wananchi hili jambo linataka kutolewa maamuzi sahihi ili lisiweze kuwaathiri wananchi na muwekezaji.” alisema Mrajisi huyo.

Hata hivyo ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuzuia Baa zote ikiwemo ya Mkunazisamaki kufanya shughuli za Sanaa mpaka pale watakapokuwa tayari kufuata taratibu na sheria zilizowekwa.

Mrajis Baraza la Sanaa, Sensa ya Filamu na Utamaduni Zanzibar (BASSFU) Juma Choum Juma akizungumza na wananchi wa shehia ya Kisauni na Maungani kuhusiana changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo upigwaji wa muziki kwa sauti kubwa katika Baa ya Oxygen iliyopo Mkunazisamaki Wilaya ya Magharibi “B “.

PICHA NA FAUZIA MUSSA –MAELEZO ZANZIBAR

Related Posts