Kigogo wa zamani Tucta afichua makubaliano ya kikokotoo

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa zamani wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), Nicolaus Mgaya amesema bado wafanyakazi wana safari ndefu ya kupata nyongeza ya kikokotoo, akitaja sababu ni Serikali kushindwa kuiwezesha mifuko ya hifadhi ya jamii kuwa na ukwasi wa kutosha.

Mgaya pia amekosoa utendaji wa Tucta akisema imeshindwa kuibana Serikali katika kudai haki za wafanyakazi likiwamo suala la kikokotoo.

Suala la kikokotoo lilianza kufukuta mwaka 2018 baada ya iliyokuwa Mamlaka ya Kudhibiti Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) kuandaa kanuni mpya zilizolenga kukipunguza kwa watumishi wa umma kutoka asilimia 50 hadi asilimia 33 na kupandisha kutoka asilimia 25 hadi 33 kwa watumishi wa sekta binafsi.

Hatua hiyo ilipigiwa kelele na watumishi wa umma, ndipo hayati Rais John Magufuli alipoivunja SSRA na kuahirisha matumizi ya kanuni hizo, akitaka zianze kujadiliwa mwaka 2023.

Julai 1, 2022, Serikali ilipeleka suala hilo bungeni, aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako alisema kikokotoo kipya kinafanya wafanyakazi wote wa Tanzania wa sekta ya binafsi na umma kutumia viwango sawa vya ukokotozi wa mafao.

Kanuni hizo zimeendelea kulalamikiwa na wafanyakazi, huku baadhi ya wabunge wakikishikia bango katika mijadala yao.

Akizungumza leo Aprili 29, 2024 katika mahojiano na Mwananchi Digital jijini Dar es Salaam, Mgaya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Tucta kuanzia mwaka 2009 hadi 2016, amesema suala hilo lilianza baada ya Serikali kuwahamisha watumishi wa umma waliokuwa wakichukua pensheni Hazina na kuwaweka katika Mfuko wa Pensheni kwa Watumishji wa Umma (PSSF).

Mgaya amesema Serikali ilitakiwa ilipe ruzuku PSSF za kuanzia kuwalipa wastaafu, lakini haikulipwa.

“Zamani wafanyakazi wa Serikali walikuwa hawachangii mafao, hivyo ilianza kuwakata michango watumishi kupunguza mzigo. Lakini Serikali pia ilitakiwa ichangie ruzuku wakati inawahamisha watumishi hao, lakini haikulipa,” amesema Mgaya.

Pia, amesema wakati huo Mfuko wa Pensheni kwa Mashirika ya Umma (PPF) na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) walikuwa wanalipa mafao asilimia 25, huku Mfuko wa Pensheni kwa Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (LAPF), GEPF na PSPF walikuwa wanalipa asilimia 50.

Amesema pia katika tathmini za kina (actuarial evaluation) zilionyesha kama mifuko hiyo itaendelea kulipa kikokotoo cha asilimia 50, mifuko itakufa.

“Tukakubaliana ifike asilimia 35 na wale wa juu washuke asilimia 35, tuendelee kuona tathmini itakavyotuambia kama tutapanda polepole mpaka tufike asilimia 50,” amesema Mgaya.

Pia, ametaja kusimama kwa ajira katika Serikali ya awamu ya tano, akisema kulisababisha kushuka kwa ukwasi wa mifuko ya hifadhi ya jamii.

“Sasa unaposimamisha ajira halafu watu wanaendelea kustaafu unategemea nini? Watu wa kuchangia hawapo, lakini wengine wanastaafu,” amesema na kuongeza kuwa, ili kikokotoo kipande, ni lazima Serikali ihakikishe ukwasi wa mifuko ya pensheni unapanda.

Mwananchi ilipomtafuta Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Deogratius Ndejembi kuzungumzia suala hilo, simu haikupokewa na hata alipotumiwa ujumbe wa maneno (sms) haukujibiwa.

Naibu wake, Patrobas Katambi alipopigiwa simu haikupokewa wala hakujibu sms, lakini Aprili 19, 2024 alipojibu hoja za wabunge, alisema tayari Serikali imeshaanza kuchukua hatua kuhusu malalamiko ya kikokotoo na majibu yatatolewa na Rais Samia Suluhu Hassan katika sherehe za Mei Mosi za mwaka huu.

Akizungumza na maofisa wa Jeshi la Polisi Septemba 4, 2023, Rais Samia aligusia changamoto za jeshi hilo ikiwamo suala la kikokotoo, akisema tatizo ni mifuko ya hifadhi ya jamii.

“Tukisema kila anayetoka bumu lako hilo hapo, bumu hilo hapo miaka miwili tu mifuko imekauka. Tuliweka hii ili kuweka longevity (uendelevu) ya mfuko, sustainability ya mifuko. Sasa kwa sababu kimepigiwa kelele sana, si tu na Jeshi la Polisi lakini na wengine tutaenda kuangalia,” alisema.

Akifananisha uongozi wa Tucta waliyokuwapo na ya sasa, Mgaya amesema wakati wao ilikuwa moto, kwa sababu viongozi wa vyama vya wafanyakazi waliokuwepo walikuwa ngangari na walikuwa wazungumzaji kwenye vikao na ajenda wanazichangamkia.

“Tucta ya sasa ipo kimya sana. Si kwamba shida hazipo, yapo matukio mengi sana yanayowahusu wafanyakazi, kwa mfano ugumu wa maisha, bei za vitu, vyakula vimepanda, umeme kukatika, yote haya hawayasemei.”

“Umeme ukikatika kama hakuna jenereta maana yake kazi hakuna, ikiendelea hivyo maana yake unafukuza wafanyakazi, hivyo ndivyo vitu ambavyo ni lazima wawasemee wafanyakazi,” amesema Mgaya.

Kuhusu kupanda bei za bidhaa, alitoa mfano wa mafuta akisema kupanda kwake husababisha gharama za usafiri kuongezeka.

“Kupanda bei ya mafuta, nauli zinapanda na watu wanaoumia; ni wafanyakazi maana wanaenda kazi kila siku, lazima watumie usafiri. Haya yote hawayasemi,” amesema Mgaya.

Kuhusu kikokotoo amesema nacho wamekaa kimya, “wanasubiri mpaka Bunge limewasemea. Hicho ndicho kitu wanapaswa waishike Serikali vizuri mpaka waje kwenye meza ya mazungumzo.”

Rais wa Tucta, Tumaini Nyamhokya alipotafutwa na Mwananchi Digital amesema hawezi kuzungumza kwa wakati huo kwa kuwa alikuwa kwenye mkutano.

Akieleza kazi walizofanya katika kipindi chao, Mgaya aliyeingia Tucta mwaka 2007 akiwa kwenye nafasi ya Naibu Katibu Mkuu na baadaye akarithi nafasi ya Katibu mkuu kutoka kwa Nestory Ngula, aliyesimamishwa na kikao cha Kamati ya Utendaji mwaka 2009, amesema walikuwa wakiibana Serikali.

“Mwaka 2010 ukaja mtafaruku wa kuitisha mgomo. Ule ulitokana na mkutano mkuu wa kazi uliofanyika mwaka 2009 ambao uliipa Serikali mambo matatu ifanyie kazi, na wasipoyafanyia tutaitisha mgomo,” amesema Mgaya.

Ameyataja mambo hayo kuwa ni nyongeza ya mshahara, kupunguzwa kodi ya mshahara kutoka tarakimu mbili kuwa moja na kuangalia mifuko ya hifadhi ya jamii.

“Baada ya miezi mitatu kukawa na kikao cha Baraza Kuu ambacho ndiyo kinatoa uamuzi baada ya mkutamo mkuu. Tukaulizana tukaona Serikali haijatupa taarifa yoyote japo tuliwaandikia barua tukidai mambo matatu. Baada ya hapo Baraza Kuu likaagiza tutoe notisi ya mgomo. Papo hapo ikateuliwa kamati ya mgomo ya watu 10 kutoka vyama 20, kwa hiyo sisi tulikuwa tunakaa kupitia mambo yanaendaje,” amesema Mgaya.

Kutokana na tishio hilo, amesema Serikali ililazimika kukutana nao ili kufanya mazungumzo.

“Serikali ilikuja kwenye meza ya majadiliano, walikuja wanasheria kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, tukakaa Wizara ya Kazi, tukajadiliana, tukatiliana saini kwamba itakapofika tarehe fulani, mifuko iwe imeundiwa mamlaka ya kuisimamia, ndipo ikaundwa Mamlaka ya Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA)”, amesema Mgaya.

“Kulikuwa pia na ajenda ya kuunganisha mifuko maana ilikuwa mingi, tukaona katika Afrika, Tanzania ilikuwa na gharama kubwa ya kuendesha mifuko hiyo, kwa sababu ilikuwa mitano ina wakurugenzi wakuu, wakurugenzi wa fedha, wakurugenzi uwekezaji, hao wote kuwahudumia gharama yake ni kubwa.”

Kutokana na suala hilo, Serikali iliiunganisha mifuko hiyo na kubaki na miwili ya PSSSF na NSSF. Amesema Serikali inaendelea kufanya vikao na Tucta kila baada ya miezi mitatu na kila mwaka kabla ya Mei mosi wanakutana na mambo yao yalikuwa yakitekelezwa.

Mgaya amesema miongoni mwa mambo yanayoidhoofisha Tucta ni mabadiliko ya katiba yao ambayo sasa katibu mkuu anachaguliwa kutoka miongoni mwa makatibu wa shirikisho hilo, tofauti na zamani nafasi hiyo ilikuwa ikiwaniwa na mwanachama yeyote.

“Ilikuwa ni kosa kubwa na sasa ndiyo wanaliona kwa wanayemchagua, anaweza kupitisha mwezi mmoja au miezi miwili haonekani makao makuu ya Tucta, yuko kwenye chama chake, hilo pengo linafanya Tucta ishindwe kufanya kazi,” amesema Mgaya.

Kuhusu vyama 19 vinavyodai kutengwa na Tucta, Mgaya amesema vinapaswa kutekeleza uamuzi wake wa kuanzisha shirikisho haraka iwezekanavyo, si ajabu kwa  nchi kuwa na shirikisho zaidi ya moja.

“Kwa mfano Afrika Kusini wana mashirikisho manne, Kenya mawili, Uganda mawili, Rwanda mawili, ukienda DRC (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo) yako sita, huko Mauritius yako manne, Namibia mawili na Zambia mawili, nchi nyingi tu,” amesema.

Related Posts