Kocha Yanga ataja siri ya Gamondi

WAKATI Yanga imebakiza pointi 12 ikiwa ni sawa na mechi nne ili kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa tatu mfululizo, kocha wa viungo wa timu hiyo, Taibi Lagrouni amefunguka siri ya ubora kwa kumtaja Miguel Gamondi kuwa ana nidhamu ya kupanga kikosi.

Timu ya Wananchi imecheza mechi tano Aprili, nne za ligi imekusanya pointi 10 na mchezo mmoja wa Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Dodoma Jiji iliyotinga hatua ya robo fainali.

Mechi walizocheza Aprili 10 ni dhidi ya Dodoma Jiji (2-0) katika Kombe la Shirikisho na za ligi ni dhidi ya Singida Fountain Gate Aprili 14 (3-0), Simba Aprili 20 (2-1), dhidi ya JKT Tanzania (0-0) na dhidi ya Coastal Union (1-0) Aprili 27.

Akizungumza na Mwanaspoti, Lagrouni alisema sio rahisi kuwa na mechi tano mfululizo na wachezaji wakacheza kwa ubora na kupata matokeo huku akiweka wazi kuwa Gamondi ndio anaibeba timu kwa kufanya mabadiliko ya wachezaji.

“Huu ni mzunguko wa pili kila timu inapambana kutafuta matokeo ili kujihakikishia kubaki msimu ujao hivyo wachezaji wamekuwa wakikutana na ugumu, kazi iliyopo kwangu ni kuhakikisha kila mmoja anakuwa timamu,” amesema na kuongeza;

“Licha ya ugumu wa mechi na mfululizo uliopo nafurahishwa na wachezaji kuhitaji kuwa timamu kwa kuzingatia kila ninachowaelekeza pia nawapa hongera nao wananirahisishia kazi yangu.” amesema.

Lagrouni amesema utimamu wa mwili kwa wachezaji ndio siri ya matokeo mazuri wanayoyapata lakini pia mbinu bora za kocha kwa kutoa nafasi kwa kila mchezaji imekuwa nafuu kwake kupata wakati mgumu wa kurudisha utimamu mara kwa mara kwa wachezaji.

“Mechi tano tulizocheza labda eneo la kipa tu ndio halijawa na mabadiliko lakini kwenye nafasi nyingi wachezaji wamepumzika walau hata kwa dakika, hii ni nzuri,” amesema na kuongeza;

“Pia kitendo cha kocha kutoa mwanya kwa wachezaji kutokana na kuona umuhimu wa mchezo hadi mchezo kwa kuzingatia utimamu wa mwili imekuwa nzuri kwa afya za wachezaji,” amesema.

YAO, AUCHO KUREJEA HARAKA
Akizungumzia kurudi haraka kwa beki Yao Kouassi na kiungo Khalid Aucho alisema wamerejea haraka kutokana na kuzingatia maelezo waliyopewa na daktari baada ya kupata shida.

“Ni kweli wamerudi haraka njia nyingi zimetumika lakini hata wachezaji wenyewe walikuwa wanazingatia walichoambiwa na daktari kwa kufuata hatua zote, walipofika kwangu kazi haikuwa ngumu nilifanya nao mazoezi na kugundua wapo tayari kwa kucheza,” amesema.

Alipoulizwa kuhusu hali ya kiungo Pacome Zouzoua alisema pia ni suala la muda tu kuanza kucheza huku akitolea mfano wa Gamondi kuzingatia kutumia wachezaji kwa kufanya mabadiliko.

“Pacome ameshaanza mazoezi suala la kutumika lipo chini ya Gamondi ambaye naheshimu mbinu zake amekuwa bora kwenye kuamini kitu anachokifanya hivyo naamini kwakuwa bado ni mchezaji wa Yanga atacheza kwenye mechi zilizobaki,” amesema.

Related Posts