Kukazia hukumu kwatajwa kikwazo utoaji haki

Dar es Salaam. Wabunge wametaka utaratibu wa kukazia hukumu mtu anaposhinda kesi uangaliwe upya kwa kupeleka muswada wa mabadiliko ya sheria bungeni.

Wabunge Mashimba Ndaki wa Maswa Magharibi na Edward Ole Lekaita wa Kiteto wameitaka Serikali ibadilishe sheria ya kukazia hukumu wakisema ni mlolongo mrefu, badala yake mtu anaposhinda kesi akabidhiwe haki yake bila kuchelewa.

Mbunge wa viti maalumu, Shally Raymond ameshangaa kwa nini adhabu ya kifo haitekelezwi na kama Serikali haiitaki ni vyema ikapeleka muswada wa mabadiliko ya sheria bungeni, ikaondolewa.

Wabunge hao wamesema jana kuwa, walipochangia mjadala bungeni wa taarifa ya mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2024/25.

Wizara hiyo ikiwa na vipaumbele 15 imeliomba Bunge kuidhinisha Sh441.2 bilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo.

Ndaki amesema mchakato wa kupata haki baada ya kushinda kesi una mlolongo mrefu kiasi cha kumkosesha mtu haki yake aliyoshinda mahakamani.

“Mchakato huu kusema ukweli, baada ya kesi kuisha; na mtu anatakiwa sasa apate haki yake ni mrefu sana, inabidi tena afungue kesi kwa msajili wa Mahakama kupata hiyo haki yake, inabidi tena aweke wakili kama ana uwezo wa kufanya hivyo, au aanze kusafiri kupata haki yake aliyopata mahakamani kwenda mahakamani tena.”

“Sasa mlolongo wote huu naambiwa uko kisheria, lakini hii sheria si inaweza kubadilishwa, kwa sababu mlolongo huu unawanyima haki wananchi wetu wengi mno.”

Ndaki amesema wananchi wanaposhinda kesi hawajui kwamba kuna kukazia hukumu na hata huo utaratibu wa namna ya kukazia hukumu na namna ulivyo kisheria ni mrefu mno, kiasi kwamba inaingiza gharama na inakatisha tamaa.

“Wananchi wetu wengi wameshindwa kupata haki yao na wengine wameaga dunia, hawapo, lakini haki yao walishinda mahakamani.”

Pia, alitoa mfano wa kesi ya mfugaji iliyokuwa Mahakama ya Rufani ambayo mfugaji huyo alishinda, “kesi ya mwisho ilikuwa ni kesi ya Mahakama ya Rufani namba 356 ya mwaka 2018 ambayo hukumu yake ilitolewa Juni, 2020. Mfugaji mmoja ambaye ng’ombe zake zilikamatwa, alishinda kesi zote mpaka Mahakama ya Rufaa, lakini mpaka leo bado hajapata haki yake.”

“Hii ya kukazia hukumu sijui na kufanya nini, hizi ni kazi za mawakili na nia ya Rais (Samia Suluhu Hassan) ni kwamba Watanzania wapate haki zao,” amesema Ole Lekaita.

Mbunge Shally amezungumzia kuhusu mlundikano wa kesi za mauaji mahakamani, “kesi hizi zimekuwepo muda mrefu na kunawaweka washitakiwa kuwa kwenye hali ya sintofahamu, mshitakiwa anaumia, familia inaumia na wale waliomshitaki pia wanaumia, kwa sababu kama ni mtu wao ameuawa. “Sasa kama ameuawa, hukumu ni auawe, nataka kujua hukumu ngapi za kifo zimetekelezeka kwa kipindi cha muda wa usoni, Tanzania hakuna au sisi tuna huruma sana au huko mahakamani hakujaenda ushahidi wa kutosha, lakini, tayari mtu ameshitakiwa kwa kuua, inachukua miaka zaidi ya 10, 20,” amesema Shally.

Akiwasilisha taarifa ya bajeti ya wizara bungeni, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Pindi Chana alitaja baadhi ya changamoto walizopata ni uhaba na uchakavu wa ofisi na makazi hasa katika Mahakama za Mwanzo na Wilaya.

Nyingine ni kuongezeka uhitaji wa huduma za kisheria ikilinganishwa na uwezo wa rasilimali fedha na watumishi, kuongezeka makosa yanayotokana na uhalifu mtandaoni.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Dk Eliezer Feleshi amejibu hoja kadhaa ikiwamo za kukazia hukumu, mlolongo wa kesi na adhabu ya kifo.

Amesema kuna maeneo Serikali imeyafanyia kazi. “Kwa mfano, kwa sasa mtu anayepeleka shauri Mahakama ya Rufani ahitaji kuomba kibali,” amesema.

Amesema jitihada zingine ambazo zimefanyika ni kupunguza milolongo ya upatikanaji wa nyaraka za mahakama kwamba sasa inapatikana kwa muda mfupi, tofauti na ilivyokuwa zamani.

Related Posts