LIGI ya Championship imefikia tamati jana kwa msimu wa 2023/2024 huku Kocha Mkuu wa Pamba, Mbwana Makata akiweka rekodi ya kipekee kwa kuipandisha timu hiyo Ligi Kuu Bara baada ya kusota kwa takribani miaka 23 tangu iliposhuka rasmi daraja.
Makata licha ya kuweka rekodi hiyo pia amejitengenezea ufalme wa kupandisha timu nyingi Ligi Kuu Bara pindi zinaposhuka kwa sababu Pamba ni ya nne kuiongoza kufanya hivyo akifuata nyayo za makocha wengine akiwamo, Fredy Felix ‘Minziro’ na Hassan Banyai.
Aliyekuwa Kocha wa Coastal Union, Juma Lazaro ndiye anayeongoza kupandisha timu Ligi Kuu akifanya hivyo mara tano baada ya kukipandisha kikosi hicho misimu miwili akianza 2011/2012 akiwa na Juma Kampira na 2017/2018 wakati wa Juma Mgunda.
Pia Lazaro aliipandisha Mgambo Shooting msimu wa 2012/2013 na African Sports mwaka 2015 akifuatiwa na Makata aliyeanza na Alliance FC (2018/2019), Polisi Tanzania (2019/2020), Dodoma Jiji (2020/2021) na msimu huu akiipandisha Pamba FC.
Wengine ni Fredy Felix ‘Minziro’ akiwa na Singida United (2017/2018), KMC (2018/2019) na Geita Gold (2021/2022) sawa na ilivyo kwa Stephen Matata aliyezipandisha Transit Camp (2004/2005), Tanzania Prisons (2011) na Mbeya Kwanza (2021/2022).
Mwingine ni Hassan Banyai aliyezipandisha Moro United (2011), Majimaji FC (2014/2015) na Njombe Mji msimu wa 2017/2018.
Akizungumzia hayo Kocha wa Pamba, Mbwana Makata alisema siri kubwa ya mafanikio yake ni kufanya kazi kwa ushirikiano na viongozi na wachezaji wa timu zote alizozipandisha kwani hilo kama halipo hawawezi kutimiza kile ambacho wamekikusudia.
“Jambo jingine mbali na hilo ni suala la uchumi pia kwa sababu kocha unaweza ukawa na mahitaji yako lakini klabu uliyopo ikashindwa kukutimizia, nashukuru msimu huu ligi imekuwa na wadhamini wengi hivyo imechangia mafanikio yetu,” alisema.