Geita. Mmomonyoko wa maadili kwa baadhi ya watumishi wa umma umetajwa kuwa ni moja ya sababu za siri za Seikali kuvuja na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii.
Hayo yamebainishwa leo Aprili 29, 2024 na Sijali Korojelo, kaimu mkurugenzi anayesimamia mafunzo kwa watumishi katika Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, kwenye hafla ya ufungaji wa mafunzo ya siku mbili kwa maofisa tarafa na watendaji kata wa halmashauri sita za Mkoa wa Geita.
Korojelo amesema kuna mmomonyoko wa maadili kwa baadhi ya watumishi wa umma na kuwa mafunzo hayo yamelenga kuikumbusha kada hiyo ya utumishi, maadili na umuhimu wa kutunza siri za Serikali, lakini pia kuwakumbusha hatua zitakazochukuliwa kwa atakayebainika kuvujisha siri.
“Ipo shida ya uvujaji wa siri za Serikali, siku hizi ni kawaida kukuta barua za siri kwenye mitandao ya kijamii na ndio maana tumeona tuwakumbushe juu ya umuhimu wa kutunza siri za Serikali na nini madhara yake kama watabainika,” amesema Korojelo.
Mafunzo hayo kwa mujibu wa Boniphace Luhende aliyezungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais (Tamisemi), yamehusisha maofisa 142 na yamefanyika kutokana na tathmini ya utendaji kazi iliyofanywa kwenye kata mbalimbali kubaini changamoto ya ukosefu wa umakini na weledi kwenye shughuli zao.
Luhende amesema miongoni mwa mada zilizofundishwa ni pamoja na kuwakumbusha majukumu yao ya msingi, sera na sheria zinazosimamia tawala za mikoa na serikali za mitaa, maadili ya utumishi wa umma, usimamizi wa miradi, utunzaji wa siri pamoja na kuwaeleza wananchi miradi ya mafanikio inayofanywa na Serikali.
Akifunga mafunzo hayo, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela, amewataka maofisa tarafa na watendaji kata kutoka kwenye utendaji kazi wa mazoea na mafunzo waliyopewa yawasaidie kupata maarifa na ujuzi.
“Ukiwa kiongozi, unapopata mafunzo, yapo mambo unayoyapata yanayokusaidia kushughulika na saikolojia za watu na namna gani ya kumudu hali, pale mwananchi anapowasilisha kwa lugha ya kukuumiza wewe.
“Yapo mafunzo ambayo yatakusaidia namna gani ya kufanya kazi na watu wa aina hiyo, maana kama kiongozi unapaswa kuwa na hekima na busara,” amesema.
Amewataka watambue kwenye maeneo yao ya kazi wao ndio wasimamizi wa miradi yote inayotekelezwa, hivyo wanapaswa kuhakikisha inatekelezwa kwa viwango vinavyotakiwa.
“Kwenye maeneo yenu, hakikisheni mikutano na taarifa za mapato na matumizi zinasomwa kwa wananchi, huu ndio utawala bora. Usipokuwepo utawala bora, ndiyo malalamiko hayaishi, mnawajibika kusimamia masuala hayo pamoja na kusikiliza kero za wananchi na mkifanya hivi maeneo yenu hayatakuwa na malalamiko,” amesema.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, mwenyekiti wa mafunzo hayo, Pilla Robert amesema mafunzo yaliyotolewa yatawasaidia kufanya kazi kwa bidii, weledi na ufanisi na kuleta matokeo chanya kwenye maeneo yao ya kazi.
Pia, ameomba mafunzo hayo yaendelee kutolewa hadi ngazi za vijiji ili kuwakumbusha watendaji wa vijiji na mitaa majukumu yao na kusaidia kwa umoja wao kwenda kwenye njia sahihi kama watumishi wa umma.