Mbolea chanzo cha mgogoro USM Alger, RS Berkane

UNAWEZA kuona kwa jicho la kisiasa mgogoro uliopelekea mechi ya pili ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baina ya RS Berkane na USM Alger kutochezwa jana kama ilivyokuwa kwa mechi ya kwanza lakini nyuma yake kuna sababu za kiulinzi na pia kiuchumi.

Sababu ya USM Alger kugomea mechi kwa vile RS Berkane walitaka kutumia jezi zenye bendera na ramani ya Morocco nyuma yake inatajwa kuwa ni uungaji mkono wa serikali ya Algeria wa harakati za eneo la Saharawi Magharibi kujiondoa kutoka katika himaya ya Morocco na kutaka kuwa taifa linalojitegemea.

Mechi ya kwanza haikuchezeka kwa vile serikali ya Algeria iliizuia RS Berkane kutumia jezi zenye bendera na ramani ya Morocco jambo ambalo lilikuwa kinyume cha taratibu za mchezo na kusababisha timu hiyo ya Morocco kupewa ushindi wa pointi tatu na mabao 3-0 huku USM Alger ikiamriwa kwenda Morocco kwa ajili ya mchezo wa marudiano.

Na jana Jumapili, USM Alger ilisusia mechi kwa vile haikuwa tayari kucheza na RS Berkane ikiwa imevaa jezi kama zile ambazo zilifanya mechi ya kwanza isichezwe.

Algeria imekuwa na mgogoro wa kisiasa na Morocco chanzo kikiwa na eneo la Saharawi.

Kumekuwa na vuguvugu la watu wa eneo la Saharawi kujiondoa chini ya himaya ya Morocco na zimekuwa zikiungwa mkono na Algeria huku serikali ya Kifalme ya Morocco ikiwa haiko tayari kuachia eneo hilo kuwa taifa huru.

Saharawi ni eneo la kimkakati la Morocco kutokana na sababu za kiusalama, shughuli za uvuvi na uwepo wa madini ya phosphate ambayo yanatumika kutengeneza mbolea.

Kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kutokana na utafiti iliofanya mwaka 2017, Morocco ndio nchi inayoongoza kwa uzalishaji wa mbolea ya phosphorus inayotokana na madini ya phosphate ikizalisha tani milioni 50 kwa mwaka ikifuatiwa na Algeria inayozalisha tani milioni 2.2 kwa mwaka.

Rungu la Caf kutua USM Alger

USM Alger itatozwa faini ya Dola 50,000 (Sh130 milioni) na kufungiwa kushiriki mashindano yote ya klabu yaliyo chini ya Caf kutokana na kosa hilo la jana.

Kanuni ya 11 ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika inafafanua kuwa timu ambayo itashindwa kucheza mchezo wa hatua ya robo au nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika itatozwa kiasi hicho cha fedha pamoja na kifungo.

“Kujitoa kwa timu ambako kutaripotiwa katika hatua ya robo fainali au nusu fainali kutaenda sambamba na kupoteza haki ya kuingia katika mashindano na faini ya Dola 50,000,” inafafanua ibara ya nane ya kanuni hiyo.

Related Posts