Dodoma. Serikali imesema katika kipindi cha Juni, 2023 hadi Machi, 2024 Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imetoa mafunzo kwa viongozi na wahadhiri 48 kutoka vyuo vikuu vitatu vilivyopo Zanzibar.
Mafunzo hayo yameelezwa yalijumuisha viongozi na wahadhiri kutoka vyuo vikuu na vyuo vikuu vishiriki 49 vilivyosajiliwa chini TCU.
Hayo yameelezwa leo Jumatatu Aprili 29, 2024 na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga alipojibu swali la msingi la Mbunge wa Donge, Mohamed Jumaa Soud.
Mbunge huyo amehoji TCU ina mkakati gani wa kuimarisha shughuli zake Zanzibar.
Kipanga amesema TCU inatekeleza majukumu yake yote katika pande zote mbili za Muungano yanayohusisha utoaji wa mafunzo kwa viongozi na wahadhiri wa vyuo vikuu vilivyopo Tanzania Bara na Zanzibar.
Mafunzo yanahusu masuala ya elimu ya chuo kikuu, ikiwemo ya uongozi na usimamizi wa vyuo.
Majukumu mengine ni uandaaji wa mitalaa inayokidhi mahitaji ya soko, mbinu bora za ufundishaji na uthibiti ubora wa elimu ya juu.
Ametoa mfano, katika kipindi cha Juni, 2023 hadi Machi 2024 viongozi na wahadhiri 48 kutoka vyuo vikuu vitatu vilivyopo Zanzibar wamepata mafunzo yaliyojumuisha viongozi na wahadhiri kutoka vyuo vikuu na vyuo vikuu vishiriki 49 vilivyosajiliwa chini ya TCU.
“TCU kila mwaka hufanya tathmini ya utekelezaji wa majukumu yake. Kutokana na tathmini hiyo, mikakati ya uboreshaji huwekwa kwa lengo la kuimarisha utekelezaji wa majukumu yake katika pande zote za Tanzania Bara na Zanzibar,” amesema.
Katika swali la nyongeza, Soud amehoji Serikali ina mpango gani wa kupanua wigo wa uwakilishi wa Zanzibar na ujenzi wa ofisi Visiwani humo ili kuimarisha uratibu.
Naibu Waziri Kipanga amesema uwakilishi katika ngazi ya utendaji kwenye TCU ni mzuri kwa pande zote za Muungano.
Kuhusu ujenzi wa ofisi, Kipanga amesema hivi sasa wanafanya kazi kwa mtandao ambao bado mtu anaweza kuifikia ofisi hiyo akiwa mahali popote ndani na nje nchi.