SIO ZENGWE: Ndio Kombe la Muungano, lakini si la kukurupushana

TANGU kuungana kwa Tanganyika na Zanzibar, michezo imekuwa ni moja ya shughuli muhimu zinazochochea kuimarika kwa Muungano kwa kukutanisha wananchi wa pande zote mbili na kuwashindanisha.

Mara zote michezo ni undugu na hutumika pia kujenga urafiki, achilia mbali faida nyingine kama za kujenga afya ya mwili na kutoa ajira kwa vijana na watu wa umri mwingine na fani tofauti.

Ndiyo maana wahenga wetu waliona umuhimu wa kuwa na mashindano ya michezo tofauti yanayojumuisha timu au klabu kutoka pande zote za Muungano ili faida hizo ziweze kunufaisha umoja wetu wa kitaifa unaopigiwa mfano sehemu nyingi duniani.

Kuna mashindano kama yale ya Pasaka ambayo mara nyingi hutokana na juhudi binafsi za wananchi ambao timu za kutoka upande mmoja wa Muungano, huzialika timu kutoka upande mwingine bila ya hata vyama vya michezo yao kuhusika kwa karibu sana.

Mashindano hayo huwa hayahitaji hata uwanja wenye vipimo vinavyokubalika au waamuzi waliopitia mafunzo ya mchezo huo au udhamini mkubwa wenye mikataba inayofunga wahusika kama ilivyom katika mashindano mengine.

Hawa huhitaji kujichangisha fedha kwa ajili ya kupata nauli na fedha za chakula na mambo mengine wawapo Bara au Visiwani na huwa hakuna bingwa ambaye anatwaa taji.

Ni Dhahiri baadhi ya watu au taasisi huandaa mashindano ambayo ni rasmi sana, yenye kanuni na zawadi za ubingwa, lakini kihistoria haya ni mashindano yanayoendeshwa kindugu na bila mizengwe yoyote, tena kwa timu ambazo wachezaji wake hawajahi kukutana hata siku moja katika maisha ya kawaida.

Lakini vyama vikaanzisha baadaye mashindano rasmi kwa ajili ya kutafuta uwakilishi wa nchi kimataifa, na katika soka kulikuwa na Ligi Kuu ya Muungano ambayo ilitoa bingwa wa nchi, ambaye alishiriki Klabu Bingwa ya Afrika, wakati mshindi wa pili alishiriki Kombe la Washindi, huku bingwa wa Kombe la FA akishiriki Kombe la CAF.

Baadaye Zanzibar ikapata uanachama wa muda Shirikisho la Soka Afrika (CAF) wakati juhudi zikifanyika kuiwezesha kuwa mwanachama wa Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa).

Hata hivyo, kanuni za Fifa zinataka mwanachama awe ni yule anayetambuliwa na Umoja wa Mataifa (UN) isipokuwa zile nchi nne waasisi zinazounda Umoja wa Falme za Uingereza (UK), yaani England, Scotland, Wales na Ireland.

Hivyo Zanzibar ikashindwa kupata uanachama huo.

Lakini ilinufaika na kitu kimoja; klabu zake ziliruhusiwa kushiriki mashindano ya klabu ya Afrika kama Klabu Bingwa ya Afrika (sasa Ligi ya Mabingwa), Kombe la CAF ambalo lilifutwa na kurudishwa baadaye na Kombe la Washindi ambalo lilifutwa.

Kwa hiyo hadi sasa klabu za Zanzibar zinashiriki mashindano ya Afrika, lakini timu ya taifa inashiriki mashindano ya ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) tu.

Ndio maana umuhimu wa Ligi ya Muungano ukapotea, ingawa kumekuwa na kilio mashindano hayo yarudishwe japo kwa sababu ya zile faida zake kwa nchi.

Kwa kujua haja hiyo ambayo imekuwepo muda mrefu, nilidhani mamlaka za soka nchini (Zanzibar na Shirikisho la Soka Tanzania, TFF) zingefanyia kazi suala hilo kwa kujiwekea kipindi kirefu ili suala hilo likiibuliwa lisiwe la kukurupuka wala kushtusha kwa kuwa maoni ya kutaka mashindano ya Muungano yarejeshwe yamekuwepo muda mrefu.

Lakini mamlaka zikatulia wala zisijiandae kwa lolote hadi mwezi huu wakati zilipogutuka na kutangaza kuwepo kwa mashindano ya Kombe la Muungano bila ya maandalizi yoyote makubwa wala kanuni kwa ajili ya kuziongoza.

Nadhani kanuni zitakuwa ni zile za kawaida zenye sentensi mwishoni inayosema “kama kuna mapungufu, kanuni za Ligi Kuu ndio zitatumika.”

Sikutegemea Kombe la Muungano lianzishwe kwa kuahirisha mechi za Ligi Kuu katikati ya msimu na kwa taarifa ya siku zisizozidi tano. Niliongea na mmoja wa wahusika wakuu wa klabu zilizoshiriki, akaniambia hata wao hawakujua kuna mashindano hayo kwa kuwa walitaarifiwa siku chache kabla ya mechi yao ya kwanza.

Hivi huku ndiko tunakoelekea? Yaani baada ya uholela wote uliokuwa unafanyika huko nyuma kabla ya wadau kujenga taratibu na kuunda vyombo vya maamuzi pamoja na misingi ya kufanya maamuzi, ndio unarejeshwa leo?

Yaani Kombe la Muungano lisiwe na misingi yoyote ya kupata timu, lisiwe na udhamini mnono, lisiwekwe hata kwenye kalenda ya shughuli za TFF kiasi kwamba liwe linajulikana wakati wa kupanga ratiba ya mashindano?

Naelewa mamlaka zinaweza kuwa zinajitetea chinichini kuwa hali hiyo imesababishwa na viongozi wa serikali kulazimisha yafanyike.

Lakini, kama ni kweli walilazimishwa, serikali ingewezaje kuingilia kama TFF na Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF) wangezingatia wito huo wa muda mrefu wa kurejesha mashindano hayo kutokana na umuhimu wake kitaifa?

Leo hii Fifa imeweka vigezo vya timu kufuzu kucheza michuano mipya ya Klabu Bingwa ya Dunia itakayofanyika Juni na Julai mwakani na kadri timu zinavyofanya vizuri kimataifa ndivyo zinavyoongeza sifa za kushiriki.

Kwa nini? Ni kwa sababu Fifa inajua umuhimu wa kuandaa mashindano mapema ili yawe pia moja ya vyombo vya kutafutia udhamini, pia kutafuta kampuni ambazo zitanunua hali za matangazo.

Unawezaje kuuza Kombe la Muungano ndani ya wiki mbili au hizo siku chache kama kiongozi huyo mwandamizi wa klabu alivyonidokeza?

Hivi idara za masoko na za mashindano ndani ya TFF zinafanya kazi gani kama si kupanga shughuli za shirikisho kwa muda mrefu na kuzitumia kama nyenzo ya kupata wadhamini na kuuza haki za matangazo ya moja kwa moja.

Ni bahati kwamba tunayo Azam Media ambayo iko tayari kurusha moja kwa moja mashindano, lakini kadri itakavyokuwa inapata maudhui ndivyo itakavyokuwa ngumu kwa shughuli holela za TFF kurushwa na Azam Media.

Ni muhimu kwa mamlaka za soka nchini na vyama vingine vya michezo kuona umuhimu huo wa kupanga shughuli zao mapema ili kutovuruga ratiba zake kwa kurupuka, pia kuwa na uhakika wa kutengeneza fedha kwa kuuza mashindano hayo kwa wadau kama wadhamini na watangazaji.

Bila kupepesa maneno, Kombe la Muungano ambalo lilishirikisha timu nne na kumalizika Jumamosi usiku kwa Simba kutwaa ubingwa, halikuwa na hadhi inayolingana na ukubwa wa jina lenyewe na umuhimu wake kwa nchi.

Ni muhimu kwa viongozi wa soka na vyama vingine vya michezo kuwa wa kwanza kufikiria mambo yanayohusu nchi na kupanga shughuli zao.

Kama wasipofanya hivyo, watajikuta wakiburuga ratiba zao kuruhusu mashindano mengine ya maadhimisho ya kitaifa kwa kuwa bado yako mengine mengi.

Related Posts