Wabunge wapaza sauti kukosekana haki mahakamani

Dodoma. Wabunge wametaka utaratibu wa kukazia hukumu pale mtu anaposhinda kesi ya madai uangaliwe upya kwa kupeleka muswada wa mabadiliko ya sheria bungeni.

Wabunge Mashimba Ndaki wa Maswa Magharibi na Edward Ole Lekaita wa Kiteto wametaka Serikali ibadilishe sheria ya kukazia hukumu, wakisema ina mlolongo mrefu, badala yake wanataka mtu anaposhinda kesi akabidhiwe haki yake bila kuchelewa.

Mbali na hilo, pia wameshangaa kwa nini adhabu ya kifo haitekelezwi na kusema Serikali haiitaki ipeleke muswada wa mabadiliko ya sheria bungeni ikaondolewa.

Wabunge hao wamepaza sauti hizo leo Aprili 29, 2024 walipochangia mjadala bungeni wa taarifa ya mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Wizara hiyo ikiwa na vipaumbele 15, imeliomba Bunge liidhinishe Sh441.2 bilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo.

Katika mchango wake, Ndaki amesema mchakato wa kupata haki baada ya mtu kushinda kesi ya madai una mlolongo mrefu kiasi cha kumkosesha mtu haki yake aliyoshinda mahakamani.

“Mchakato huu kusema ukweli, baada ya kesi kuisha na mtu anatakiwa sasa apate haki yake ni mrefu sana, inabidi tena afungue kesi kwa msajili wa mahakama kupata hiyo haki yake, inabidi tena aweke wakili kama ana uwezo wa kufanya hivyo, au aanze kusafiri kwenda mahakamani tena kupata haki yake aliyopata mahakamani,” amesema.

“Sasa mlolongo wote huu naambiwa uko kisheria, lakini hii sheria si inaweza kubadilishwa, kwa sababu mlolongo huu unawanyima haki wananchi wetu wengi mno,” amesema.

Amesema wananchi wanaposhinda kesi hawajui kwamba kuna mambo ya kukazia hukumu na hata huo utaratibu wa namna ya kukazia hukumu na namna ulivyo kisheria ni mrefu mno, kiasi kwamba unaingiza gharama na unakatisha tamaa.

“Wananchi wetu wengi wameshindwa kupata haki zao na wengine wameaga dunia, hawapo, lakini haki yao waliishinda mahakamani,” amesema.

Akizungumzia pia hilo, Ole Lekaita ametoa mfano wa kesi ya mfugaji iliyokuwa Mahakama ya Rufani ambayo mfugaji huyo alishinda lakini haki yake ikacheleweshwa.

“Kesi ya mwisho ilikuwa ni kesi ya Mahakama ya Rufani namba 356 ya mwaka 2018 ambayo hukumu yake ilitolewa Juni 2020. Mfugaji mmoja ambaye ng’ombe wake walikamatwa, alishinda kesi zote mpaka Mahakama ya Rufaa, lakini mpaka leo bado hajapata haki yake.”

“Hii ya kukazia hukumu sijui na kufanya nini, hizi ni kazi za mawakili na nia ya Rais  ni kwamba Watanzania wapate haki zao,” amesema Ole Lekaita.

Mbali na hilo, mbunge Shally Raymond (Viti Maalumu) yeye alizungumzia kuhusu mlundikano wa kesi za mauaji mahakamani kuwa nao unanyima haki za watu.

“Kesi hizi zimekuwepo muda mrefu na kunawaweka washtakiwa kwenye hali ya sintofahamu, mshtakiwa anaumia, familia inaumia na wale waliomshtaki pia wanaumia sana, kwa sababu kama ni mtu wao ameuawa,” amesema.

“Sasa kama ameuawa, hukumu ni auawe, nataka kujua hukumu ngapi za kifo zimetekelezeka…, Tanzania hakuna au sisi tuna huruma sana au huko mahakamani hakujaenda ushahidi wa kutosha, lakini, tayari mtu ameshtakiwa kwa kuua, inachukua miaka zaidi ya 10 au 20,” amesema.

“Sisi watu wa kawaida, nashangaa na ninajiuliza kama hii hukumu ya kifo haitekelezeki, kwa nini ipo. Muswada si uletewe hapa na Serikali tuibadili,” amesema.

Mbunge huyo amesema, “Kusema Tanzania haitekelezi au haiko tayari kutoa hukumu ya kifo. Mimi jambo hili nalisema kwa uchungu, lakini kwa vile jambo liko mahakamani si ruhusiwi kutamka ila nina mtu wa karibu.”

“Hata mimi sitaki kuua, lakini tujue nini kinachoendelea tunapomweka mtu anakaa mahabusu miaka nenda nurudi, na ninyi mnatuambia hapa ‘justice delayed is justice denied’ (Haki iliyocheleweshwa ni haki iliyonyimwa), iko wapi hiyo ‘justice’ (haki) hapa,” amehoji.

Kabla ya wabunge hao kuchangia, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Pindi Chana aliwasilisha bajeti ya wizara yake bungeni hapo, alitaja baadhi ya changamoto za mahakama, ikiwemo uhaba na uchakavu wa ofisi na makazi hususani katika Mahakama za Mwanzo na Wilaya.

Changamoto zingine ni kuongezeka kwa uhitaji wa huduma za kisheria ikilinganishwa na uwezo wa rasilimali fedha na watumishi, kuongezeka kwa makosa yanayotokana na uhalifu kwa njia ya mtandao ikilinganishwa na uwezo wa kuyabaini.

Zingine ni gharama kubwa za kuendesha mashauri ya nje ya nchi ikilinganishwa na bajeti iliyotengwa, jambo ambalo linasababisha kuomba kupatiwa fedha nje ya bajeti ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.

Pia alitaka upungufu wa mawakili wa Serikali wenye ubobezi katika maeneo ya gesi, mafuta, uwekezaji, anga, madini, uchumi wa buluu, na maeneo mengine ya kimkakati, hali inayosababisha kupungua kwa ufanisi katika uendeshaji, usikilizwaji wa kesi na upekuzi wa mikataba.

Related Posts