Wabunifu teknolojia za elimu “njooni mchukue mkwanja”

Dar es Salaam. Wabunifu wa teknolojia ya elimu nchini wametakiwa kuwasilisha maombi ya fedha na mafunzo kwa ajili ya kuendeleza bunifu zao ili kuleta suluhu za kielimu nchini.

Akizungumza jana Aprili 28, 2024 wakati wa kutambulisha mradi wa wa mafunzo hayo uitwao Mastercard Foundation EdTech Fellowship, Mtendaji Mkuu wa Sahara Ventures, Jumanne Mtambalike amesema lengo ni kuwaunga mkono vijana wa Tanzania, wenye mawazo ya kiubunifu ambayo yanatumia teknolojia kwenye sekta ya elimu.

Amesema mradi huo utakuwa wa miaka mitano na miaka mitatu ya kwanza kila mwaka watakuwa wanawasaidia vijana 12 kwenye kampuni zao, ili kuhakikisha wanaweza kuendeleza sekta ya elimu na makampuni ya vijana kutengeneza ajira.

“Lengo letu ni kuunga mkono vijana wenye bunifu zikijumusha teknolojia ya mapinduzi makubwa ya nne ya viwanda (IA), kwa hiyo kila kijana ambaye wazo lake linatumia teknolojia na ubinufu hata kama umetengeneza kitu kinachorahisisha watoto kusoma na kujifunza, unaweza kuomba fedha,” amesema.

Amebainisha kuwa maombi yote yanafanyika kwa njia ya mtandao wa EdTech.saharaventure.com na endapo mtu atakidhi vigezo anaweza kupata ufadhili huo.

“Hatua vya kwanza wote wataomba kwa njia ya mtandao, hatua ya pili kupitia  walioomba na kuwachuja wabaki wachache na tatu tutajadili na wadau kuangalia ni wapi wana uwezo wa kukuza na tutakaa na washirika wetu kuangalia wanaokidhi kupata hizo fedha,” amesema.

Mtambalike alisema mbali na fedha pia watasaidiwa kwenye mambo manne kama vile bidhaa wanazotengeneza, namna ya kukuza biashara, namna wanavyoweza kufanya kazi vizuri na Serikali na masuala ya masoko ikiwemo kupata wateja.

“Natoa wito kwa vijana kuwa kuna taasisi nyingi zinasaidia vijana kama Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech) ipo kwa ajili yao, vijana watoke waende kutoa mawazo yao,” amesema Mtabalike.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Menejimenti ya Maarifa wa Costech, Samson Mwela amesema lengo la mradi huo ni kuboresha miundombinu ya bunifu za vijina na hilo linaunga mkono juhudi za Serikali zinazoendelea za kukuza kampuni za ndani.

“Ni fursa muhimu kwa wabunifu wenye teknolojia za elimu kuwasilisha maombi yao kwa hizi juhudi zinazofanyika zitaleta suluhisho katika kutekeleza sera ya elimu.

“Tumekuwa tukiwawezesha wabunifu, hasa vijana, na tunaendelea kuwaunga mkono na hapa kuna wadau wamepata fedha, hii ni fursa nzuri kwa ajili ya kuendeleza elimu kwa njia ya teknolojia.”

Related Posts