BARAZA la Michezo la Taifa (BMT) limewataka waogeleaji wa timu ya Taifa kuhakikisha wanafanya vema kwenye mashindano ya kuogelea ya Afrika (Africa Aquatics Swimming Championship) yatakayoanza kesho Aprili 30 hadi Mei 2 mwaka huu nchini Angola.
Mashindano hayo yana lengo la kuwania kufuzu michuano ya Olimpiki itakayofanyika Julai 26 hadi Agosti 11 nchini Ufaransa na Tanzania inawakilishwa na Sofia Latiff, Collins Saliboko pamoja na Hilal Hilal kwenye mashindano hayo ya Angola.
Akizungumza wakati akikabidhi bendera ya Taifa timu hiyo ofisa michezo wa baraza hilo Charles Maguzu amesema ana imani kubwa na waogeleaji kwenye mashindano hayo kutokana na maandalizi waliyoyafanya.
“Mnakwenda kuiwakilisha Tanzania katika mashindano hayo, nendeni mkapambane kuhakikisha mnashinda mnaipeperusha bendera ya Taifa letu kwa kupata medali za ushindi, Watanzania tupo nyuma yenu,” amesema Maguzu.
Amesema anawapongeza kupata nafasi adimu ya kuteuliwa kwenye timu ya Taifa kwenda kuiwakilisha nchi yetu, na kuipongeza kamati ya utendaji ya chama cha mchezo wa kuogelea Tanzania (TSA) kwa juhudi inayofanya kuinua vipaji vya vijana kupitia mchezo huo ambao kwa sasa unazidi kushika kasi.
“Ninaipongeza kamati ya utendaji kwa kutoa fursa kwa makocha wenu kwenda nje ya nchi kunapotokea mashindano ya kimataifa ili kila mmoja akaonyeshe uwezo wake tofauti na vyama vingine vimekuwa vitoa fursa kwa mtu mmoja jambo ambalo linavunja moyo,” amesema.
Kwa upande wake rais wa chama hicho, David Mwasyoge alisema anawapongeza waogeleaji hao kutokana na ubora wanaozidi kuuonyesha katika mashindano mbalimbali ambayo wamekuwa wakiyafanya na kuweka wazi wamefanya kazi kubwa mpaka kufika walipo sasa.
Kocha mkuu wa timu hiyo Yusuph Isiki amesema ameandaa waogeleaji wake akiwa na matumaini ya kwenda kupata matokeo mazuri.
Wakati huohuo, nahodha wa timu hiyo, Sofia Latiff ambaye alizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake alisema malengo yao ni kwenda kuvunja rekodi zao ili waweze kupunguza muda licha ya kutarajia upinzani mkubwa.