Wazazi wametakiwa kuwa na tabia ya kufuatilia mienendo ya watoto wao ikiwa njia mojawapo ya kuwalinda dhidi ya ukatili wanaoweza kufanyiwa na baadhi ya watu waliokosa maadili mema..
Akizungumza katika hafla ya maadhimisho ya miaka 25 ya kuanzishwa kwa Huduma ya Mtoto na Kijana Tanzania iliyo chini ya shirika la Compassion international Tanzania kwa kushirikiana na makanisa ya Anglikana,T.A.G, KKKT, Morovian na FPCT afisa maendeleo ya jamii halmashauri ya mji wa Korogwe Bw.Fredrick Kitundu amesema ni wajibu wa kila mzazi kufuatilia mwenendo wa mtoto wake .
“Chonde chonde wazazi tumekuwa na tabia ya kitofatia mienendo ya watoto wetu na badala yake tumekariri tu kuwa watoto wanatoka wanaenda shule na kurudi hivyo ni vyema kufatilia wameenda shule na wamefika salama kwani wakati mwengine hata walimu wanaweza kuwa changamoto kwenye usalama wa watoto hivyo kama wazazi tutimize wajibu wetu”
Akisoma taarifa kwa mgeni rasmi mtaalamu wa fedha na mawasiliano wa kituo cha FPCT Mombo ndugu Emanuel Cosmasi amesema mpaka sasa vituo vya Korogwe pekee vinahudumia watoto zaidi ya 1400 katika Nyanja za kiuchumi,kielimu,kiroho na kijamii huku Canon Jackson Matuga akisema kuwa katika kuhudumia watoto hao hawachagui dini lakini wananagalia uhitaji wa mtoto.
“Katika huduma hii tunayo itoa kwa watoto hawa hatuangalii dini bali tunaangalia uhitaji wao kama watoto wa kitanzania hivyo tunaomba serikali kushirikiana nasi pale tunapo hitaji msaada pindi watoto hawa wanapo pata changamoto yeyote”
Kauli mbiu ya Maadhimisho haya ni MALEZI BORA KWA ULINZI WA MTOTO ikiwa ni kuhamasisha ulinzi wa watoto katika jamii na itambulike kuwa maadhimisho haya yamekwenda sambamba na zoezi la upandaji miti kwenye maeneo ya serikali ikiwemo vituo vya afya.