Yanga yafanya uamuzi mgumu kwa Lomalisa, Kibabage

UONGOZI wa klabu ya Yanga umefanya uamuzi mgumu kwa nyota wake wawili wa nafasi ya ulinzi ya beki ya kushoto, Joyce Lomalisa Mutambala na Nickson Kibabage kwa kumbakisha kikosini staa huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar ambaye anacheza kwa mkopo kutokea Singida Fountain Gate akichukua nafasi ya Mcongo huyo anayetimka mwisho wa msimu.

Kibabage alikuwa Yanga kwa mkopo ambao unaisha mwisho wa msimu huu lakini viongozi wa Yanga hawajakubali kumpoteza beki huyo damu changa ambaye anafunga na kutoa asisti za mabao.

Ipo hivi; Uongozi wa Yanga umekubaliana kuachana na Lomalisa na kumalizana na Singida Fountaine Gate kwa kumnunua Kibabage na kumpa mkataba mpya wa miaka mitatu.

Kibabage alikuwa amebakisha mwaka mmoja katika mkataba wake na Singida Fountaine Gate hivyo Yanga wamefanya biashara na walima zabibu hao kwa kujimilikisha beki huyo.

“Uamuzi uliofanyika ni kubaki na Kibabage kutokana na umri wake na ni mchezaji ambaye ameonyesha mchango mkubwa tangu tumemchukua kutoka Singida Fountaine Gate,” kimesema chanzo chetu na kuongeza;

“Kuachana na Lomalisa sio kwamba ni mchezaji mbaya, ni mzuri lakini yeye pia kaamua kuondoka na kwenda kujaribu maisha mengine nje ya Yanga.”

Mwanaspoti lilimtafuta Ofisa Habari wa Singida Fountaine Gate, Hussein Masanza ambaye amekiri Yanga kufika mezani kwaajili ya mazungumzo juu ya kumnasa beki huyo.

“Yanga wameonyesha kuvutiwa na beki huyo kwani wamerudi mezani kutaka kummiliki wao sio kuendelea kucheza kwa mkopo kama ilivyo sasa,” amesema na kuongeza;

“Ni kweli wamekuja na mazungumzo kati ya pande zote mbili yanakwenda vizuri mambo yakienda kama tulivyopanga basi taarifa itatolewa kwaajili ya kuujulisha umma juu ya mchezaji huyo.”

Kibabage ambaye hadi sasa ndani ya kikosi cha Yanga ametoa pasi tatu zilizozaa mabao alijiunga na timu hiyo Julai mwaka jana na baada ya mkataba wake wa miezi sita kuisha walimuongeza miezi mingine sita ili kutimia mwaka na Julai mwaka huu ndio unamalizia.

Related Posts