Licha ya uharibifu unaotokea Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kupitia kitengo cha dharura imekuwa ikirudisha mawasiliano kwenye maeneo ambayo mawasiliano yamekatika kutokana na uharibifu.
Waziri wa Ujenzi Mhe Innocent Bashungwa ameyasema hayo tarehe 29 Aprili 2024 katika Manispaa ya Kigamboni wakati alipotembelea na kukagua barabara ya Kibada-Mwasonga-Kimbiji akiwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili Jijini Dar es salaam
Amesema zoezi la kufungua miundombinnu ya barabara limefanikiwa kutokana na serikali ya awamu sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuiwezesha kibajeti TANROADS kupitia kitengo cha dharura ili kurahisisha shughuli za kiuchumi na utoaji wa huduma.
Waziri Bashungwa amewahakikishia wananchi kote nchini kuwa hakuna barabara ambayo mawasiliano yatakatika kutokana na mvua kisha ikaachwa bila ya mawasiliano yake kurudishwa kwa haraka.
Kuhusu ujenzi wa barabara katika wilaya ya Kigamboni Waziri Bashungwa ameeleza kwamba, serikali ya awamu sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeridhia ujenzi wa barabara ya kutoka Kibada kwenda Mwasonga hadi Kimbiji yenye urefu wa kilometa 41.
“Awali ujenzi wa barabara ya Kibada kwenda Mwasonga hadi Kimbiji yenye urefu wa kilomita 41, ilitakiwa iishie hapo, lakini kutokana na maombi yaliyoletwa na mbunge wenu (mbunge wa Kigamboni) serikali imeridhia na hivyo tumeongeza kilometa 10 na kufanya ujenzi wa barabara hiyo itakuwa ni kilometa 51 kumalizia kipande chote kiluchobakia katika barabara hii” Amesisitiza Waziri Bashungwa
Amepongeza hatua za haraka zinazoendelea kuchukuliwa na TANROADS, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es saklaam pamoja na TARURA katika kukabiliana na athari za miundombinu ya barabara na madaraja zilizotokana ana mvua za El-Nino
Kwa upande mwingine, Waziri Bashungwa ameagiza kuundwa kwa timu maalumu na kisha kupelekwa katika eneo la Magogoni lililopo kata ya Tungi wilayani Kigamboni kwa ajili ya kufanya usanifu na kisha kuja na majawabu ya juu ya nini kifanyike ili kutatua changamoto ya maji kuzingira makazi ya wananchi wa eneo hilo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema mkoa huo unahitajika kufumuliwa kwenye mifumo imara na thabiti ya kusafirisha maji ya mvua lengo likiwa ni kuondoa athari zinazotokana na mafuriko ikiwemo wananchi kupoteza maisha.
Mkuu huyo wa Mkoa ameendelea kwa kusema kuwa, watu wengi wamejenga juu ya mifumo hiyo ya kusafirisha maji ya mvua hivyo kama mkoa watafanya usanifu kupata suluhu ya changamoto ya mafuriko.
Akizungumza kwa niaba ya wanachi, mbunge wa jimbo la Kigamboni Dkt. Faustine Ndugulile amesema, kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya kutoka Kigamboni kuelekea Mwasonga hadi Kimbiji itakuwa ni faida kubwa kwa wakazi wa Kigamboni kwani inatumiwa na watu wengi na inapita kuelekea kwenye viwanda zaidi ya 10.
Dkt. Ndugulile ameongeza kuwa, barabara hiyo inapitisha magari zaidi ya 1,000 madogo kwa makubwa yenye uzito tofauti hivyo ni barabara muhimu kiuchumi na kwa shughuli za uzalishaji.
Kando na hayo, Ndugulile ametoa ombi kwa mkandarasi anayejenga barabara hiyo pia kujielekeza kwenye ujenzi wa mifereji ya maji kwani imekuwa ni changamoto kubwa katika barabara za Kigamboni.