Bashe azindua Bodi ya Mkonge, yaahidi kufanya kazi kwa weledi

Na Ramadhan Hassan,Dodoma

WAZIRI wa Kilimo,Hussein Bashe amezindua Bodi ya Mkonge Tanzania huku akiitaka kufanya kazi kwa bidii na kuwasaidia wakulima wa zao hilo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Jumatatu Aprili 29,2024 jijini hapa,Waziri Bashe ameipongeza bodi mpya kwa kuaminiwa na Rais Samia Suluhu Hassan huku akiitaka kufanya kazi kwa ushirikiano kwani atawapima kwa malipo ya wakulima.

“Kwanza niwapongeze Bodi mpya kwa kuaminiwa na Rais,mimi nitawapima kwa malipo ya wakulima kuyapata kwa wakati,”amesema Waziri Bashe.

Kwa upande wake Mwenyekiti aliyemaliza muda wake,Mariamu Nkumbi amesema katika kipindi cha uongozi wao wamefanikiwa kurejesha mali za bodi kama jengo,wamekarabati majengo,idadi ya wafanyakazi imeongezeka.

Pia amesema fedha zimeongezeka,wamehamasisha zao la mkonge katika mikoa 13,wamesambaza mbegu katika Wilaya 16.

“Hivi karibuni kuna mikoa itaanza kulima mkonge.Mafanikio tuliyapata ni pamoja na jengo la mkonge kurudishwa kwani lilibinafsishwa.Tumefanikiwa pia kurejesha baadhi ya nyumba,”amesema Nkumbi.

Naye,Mwenyekiti mpya wa bodi hiyo,Theobald Thabi amemshukuru Rais Samia kwa nafasi aliyowapatia katika kuongoza bodi hiyo.

Amesema zipo changamoto kadhaa ambapo ameahidi kwa kushirikiana na wenzake watajitahidi kuzitatua.

“Tunaahidi kufanya kazi kwa weledi mkubwa,”amesema mwenyekiti huyo mpya wa bodi.

Related Posts