Bunifu 42 za Kitanzania tayari kwenda sokoni

Dodoma. Bunifu na teknolojia 42 kati 283, zilizoibuliwa kupitia Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (Makisatu) na kuendelezwa kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech),  zimefikia hatua ya kuingia sokoni.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Omary Kipanga amesema hayo leo Jumanne Aprili 30, 2024 alipokuwa akijibu swali la msingi la Busokelo Atupele Mwakibete.

Mbunge huyo amehoji Serikali imejipangaje kukuza vipaji kwa Watanzania waliogundua teknolojia mbalimbali hapa nchini.

Amesema Serikali inatambua umuhimu wa elimu, ujuzi na ubunifu katika kumwezesha mtu kumudu mazingira yake ikiwamo kupata mahitaji ya kijamii na kiuchumi.

Amesema kwa kutambua umuhimu wa kukuza ubunifu na ugunduzi katika kuongeza kasi ya maendeleo nchini, Serikali imeandaa mwongozo wa kitaifa wa kutambua na kuendeleza ugunduzi, ubunifu na maarifa asilia wa mwaka 2018.

Amesema mwongozo huo unasaidia Serikali na taasisi husika kutoa huduma bora kwa wananchi wanaojishughulisha na mambo ya teknolojia na ubunifu wakiwamo wagunduzi wa teknolojia mbalimbali.

Kipanga amesema Serikali imeanzisha mashindano ya Makisatu kwa lengo la kuibua na kuendeleza bunifu na teknolojia zinazozalishwa nchini.

“Mathalan, bunifu na teknolojia 283 zilizoibuliwa kupitia Makisatu zinaendelezwa na Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ambapo bunifu 42 kati ya hizo zimefikia hatua ya kuingia sokoni,” amesema.

Katika maswali ya nyongeza, mbunge wa Chunya, Masache Kasaka amehoji Serikali imejipangaje katika kuendeleza bunifu hizo na je haioni haja kuweka mitaala ya ubunifu ili kuendeleza wabunifu

Kipanga amesema Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika eneo la ubunifu na kuwa wameanzisha mfuko wa kuhakikisha wanakusanya fedha za kufadhili bunifu hizo.

Amesema mwaka 2022/23 jumla ya Sh64.9 bilioni zimetolewa kwa ajili kuendeleza bunifu mbalimbali nchini.

Related Posts