Na Jane Edward, Arusha
Mkuu wa mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda amesema dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kuwa Kila mwananchi wa Arusha ananufaika na sekta ya Utalii.
Ameyasema hayo wakati wa Kongamano la uwekezaji kwenye sekta ya Utalii uliowakutanisha wadau wa sekta hiyo Makonda amesema washiriki zipo jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali ili kuweka mazingira mazuri ya wananchi kuweza kunufaika na fursa ya Utalii mkoani Arusha.
Amesema Mkoa umewekeza nguvu kubwa zaidi katika suala la Ulinzi na usalama ili kuhakikisha wageni na watalii wanaifurahia Arusha na kutoa fursa kwa wawekezaji na wafanyabiashara kufanya shughuli zao kwa uhuru zaidi.
Akizitaja hatua ambazo amezichukua katika kutimiza maelekezo ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan katika kukuza Utalii Mkoani Arusha, Mhe. Makonda amesema tayari serikali ya Mkoa imeanza kufunga Kamera za ulinzi na taa za barabarani kwenye maeneo mbalimbali ya mkoa na hadi kufikia mwezi wa saba mwaka huu, Mkoa wa Arusha anataka uwe mkoa unaoongoza kwa kuwa na kamera na Taa nyingi kuliko mkoa mwingine wa Tanzania.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha Uwekezaji nchini Tanzania TIC Bwana Gilead Teri amesema serikali imetoa msahama wa ushuru kwa asilimia Mia moja kwa bidhaa na malighafi nyingi kwa wanaohitaji kujenga viwanja vya michezo nchini Tanzania.
Aidha Mkurugenzi huyo pia ametaja bidhaa nyingine kuwa ni pamoja na Mashine za kufua,Magari ya huduma pamoja na Vifaa vya kukatia nyasi zinazotumika viwanjani.
TIC imetoa taarifa hiyo na kuwataka wawekezaji na watanzania wenye mahoteli kufuatilia misahama na punguzo la kodi na tozo zinazotolewa na serikali ya awamu ya sita kama sehemu ya kuvutia wawekezaji kuwekeza kwenye sekta mbalimbali nchini Tanzania.
Teri ametumia kongamano hilo pia kuhimiza ujenzi wa viwanja vya michezo kwenye Hoteli zilizopo mkoani Arusha kama sehemu ya maandalizi ya Michuano ya AFCON 2027 itakayochezwa mkoani Arusha na kushirikisha timu za mataifa za mpira wa miguu kutoka barani Afrika.