Gamondi: Pacome atacheza | Mwanaspoti

KOCHA Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi ameibuka na kusema kiungo wake, Pacome Zouzoua yupo tayari kuanza kucheza na kesho Jumatano kuna uwezekano akampa nafasi, lakini itategemea na mazoezi ya mwisho leo jioni.

Kauli ya Gamondi imekuja wakati kesho Yanga ikiwa na mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Tabora United utakaochezwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam kuanzia saa 2:15 usiku.

Mara ya mwisho Pacome kuonekana uwanjani akiitumikia Yanga ilikuwa Machi 17, mwaka huu walipofungwa mabao 2-1 na Azam katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam na siku hiyo aliumia na kutolewa uwanjani.

Baada ya hapo, Pacome ambaye amehusika katika mabao 11 kwenye ligi msimu huu akifunga saba na asisti nne, amekosekana kwenye mechi saba za michuano yote.

Akizungumzia utayari wa Pacome kucheza mechi ya kesho dhidi ya Tabora United, Gamondi amesema: “Anaweza kuwepo kwa sababu hivi sasa ameanza kufanya mazoezi ya kawaida, tutaangalia katika mazoezi ya leo jioni nini kitatokea lakini inawezekana akacheza.”

“Kama tusingekuwa na mechi hii (dhidi ya Tabora United), basi uhakika mechi ijayo ya ligi (Mei 5 dhidi ya Mashujaa) angeanza kucheza angalau kwa dakika 30.”

Related Posts