Hamas na Fatah wazungumza na kulenga kufikia maridhiano – DW – 30.04.2024

Makundi hasimu ya wapiganaji wa Kipalestina ya Hamas na Fatah wameeleza nia yao ya kisiasa ya kutaka  maridhiano kwa njia ya mazungumzo walipokutana mjini Beijing. Hayo yameelezwa hii leo na msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa China Lin Jian:

“Kutokana na mwaliko wa China, wawakilishi wa kundi la Fatah na Hamas waliwasili Beijing hivi karibuni na kubadilishana mawazo, kufanya mazungumzo ya kina na ya wazi juu ya kukuza maridhiano baina ya Wapalestina. Pande hizo mbili zilielezea kikamilifu nia yao ya kisiasa ya kufikia maridhiano. Kupitia mazungumzo na mashauriano, tulijadili masuala mengi mahususi na kufikia maendeleo chanya.”

Soma pia: Vita vya Israel-Hamas: Umaarufu wa Fatah wazidi kushuka

Kwa muda sasa, makundi hayo mawili yameshindwa kumaliza mizozo yao ya kisiasa tangu wapiganaji wa Hamas walipoifurusha Fatah kutoka Ukanda wa Gaza wakati wa vita vya muda mfupi vya mwaka 2007.

Hatua ya makubaliano ya usitishwaji mapigano

Cairo | Rais Abdel Fattah el-Sisi akiwa na Mkurugenzi wa CIA William J. Burns
Rais wa Misri Abdel Fattah el-Sisi akimpokea kwa mazungumzo Mkurugenzi wa Idara ya Ujasusi ya Marekani CIA William J. Burns na maafisa wengine katika mazungumzo ya kujadili mpango wa usitishwaji mapigano huko Gaza: 07.04.2024Picha: Presidency of Egypt/Handout/Anadolu/picture alliance

Maafisa wa kundi la Hamas wameondoka mjini Cairo baada ya mazungumzo na maafisa wa upatanishi wa Misri kuhusu pendekezo jipya la kusitisha mapigano huko Gaza. Kituo cha Televisheni cha Al-Qahira News, ambacho kina mafunganamo na idara ya ujasusi ya Misri, kimesema ujumbe wa Hamas utarejea mjini Cairo na jibu rasmi la maandishi kuhusu pendekezo hilo, bila hata hivyo kuelezea wazi siku hiyo.

Soma pia: Miito ya usitishwaji mapigano Gaza yatolewa

Mataifa matatu wapatanishi katika mzozo huu ambayo ni Misri, Marekani na Qatar yamekuwa yakijaribu katika wiki za hivi karibuni kuyafufua mazungumzo hayo yaliyokwama. Hamas inatakiwa kutoa jibu la kuafiki au la kuhusu mpango wa usitishwaji mapigano kwa siku 40, sambamba na kuachiliwa kwa mateka wa Israel na wafungwa wa Kipalestina wanaoshikiliwa katika jela za Israel.

Hofu ya Israel kuhusu uwezekano wa mashtaka ya ICC

Siku ya Jumatatu, Israel ilielezea wasiwasi wake kuhusu taarifa kwamba Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC  imekuwa katika maandalizi ya kutoa waranti wa kukamatwa kwa baadhi ya maafisa wa serikali ya Tel-Aviv kwa tuhuma zinazohusiana na mienendo yao katika vita dhidi ya kundi la Hamas vilivyodumu karibu miezi saba sasa.

Urusi imeituhumu Marekani kwa kile ilichosema kuwa ni undumilakuwili kwa kupinga uchunguzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kuhusu Israel lakini inaunga mkono waranti wa Mahakama hiyo wa kukamatwa Rais Vladimir Putin.

Uholanzi | The Hague| Jengo la Mahakama ya ICC
Jengo la Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC mjini The Hague nchini UholanziPicha: Vincent Isore/IP3press/imago images

Msemaji wa Ikulu ya White House Karine Jean-Pierre alisema siku ya Jumatatu kuwa Marekani haiungi mkono uchunguzi wa ICC dhidi ya Israel na kusisitiza kwamba Mahakama hiyo haina mamlaka hayo.

Soma pia: Mwendesha mashtaka mkuu wa ICC aihimiza Israel na kundi la Hamas kuheshimu sheria ya kimataifa

ICC ambayo inaweza kuwashtaki watu binafsi kwa uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya ubinadamu na mauaji ya kimbari, imeanzisha uchunguzi dhidi ya kundi la Hamas kufuatia shambulio lao la Oktoba 7, lakini pia inawachunguza maafisa wa jeshi la Israel kufuatia operesheni yao ya kulipiza kisasi huko Gaza ambayo kwa sasa tayari imekwishasababisha vifo vya zaidi ya watu 34,500.

Idadi hiyo ya vifo imekuwa ikitolewa na Wizara ya Afya inayodhibitiwa na Hamas ambayo imeorodheshwa na Umoja wa Ulaya, Marekani, Ujerumani na mataifa kadhaa ya Magharibi kuwa kundi la kigaidi.

(Vyanzo: Mashirika)

 

Related Posts