Jamii yaombwa kusaidia matibabu watoto wenye mtindio wa ubongo

Dar es Salaam. Wananchi, mashirika ya umma na binafsi wameombwa kuchangia kampeni kuwasaidia watoto wenye mtindio wa ubongo walio chini ya uangalizi wa Hospitali ya CCBRT.

Hatua hiyo inaelezwa itasaidia kuleta mabadiliko kwa watoto chini ya miaka mitano wenye mtindio wa ubongo.

Imeelezwa kuna changamoto ya vifaatiba kwa ajili ya matibabu ya watoto hao hospitalini hapo, huku wazazi wakishindwa kugharimia baadhi wakiwa wamekimbiwa na wenza wao.

Akizungumza leo Aprili 30, 2024, Ashura Hamisi amesema wanapata matibabu bure kwa watoto wao wenye miaka chini ya mitano lakini changamoto iliyopo ni kumudu gharama za vifaatiba.

“Mzazi mwenzangu baada ya kugundua nimejifungua mtoto mwenye mtindio wa ubongo alinikimbia, hivyo nalea mtoto mwenyewe. Hapa nimeambiwa vifaatiba anavyotakiwa kutumia gharama yake ni Sh400,000 ambayo sina uwezo nayo,” amesema Ashura.

Akizungumzia matibabu, Mariam Msiga, mkazi wa Mkuranga amesema anashindwa kuhudhuria mazoezi mara kwa mara kwa sababu bima yake imeisha na hana vifaatiba vya kumwezesha mtoto kufanya mazoezi akiwa nyumbani kutokana na kushindwa kumudu gharama.

“Bima ya mtoto wangu imeisha kwa hiyo tunajikuta tunachangishana familia kwa ajili ya kupata pesa ya kumleta mtoto hospitali, anatakiwa kufika kila siku kwa ajili ya mazoezi, lakini nimejikuta nikipitiliza hadi miezi miwili na mwanangu kila baada ya wiki anapata homa,” amesema Mariam.

Mtaalamu wa viungo, Nerijo Mbilu amewataka wazazi kuwapeleka hospitali mapema watoto wenye mtindio wa ubongo ili kupata matibabu na kusaidiwa kutengemaa kwa wakati.

“Akipata matibabu mapema inasaidia kwa sababu ubongo unaendelea kukua, hivyo anaweza kupata matibabu ya makuzi katika umri unaohitajika mapema zaidi,” amesema Nerijo.

Ametoa rai kwa wazazi kuwa na tabia ya kuwachunguza watoto kuona mabadiliko kwa haraka na kuacha kuamini kitu kinachotokea kwa mtoto ni ushirikina.

Amesema matatizo yanayotokea kwa watoto yanasababishwa na vitu vingi.

Kutokana na changamoto wanazopitia, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Creditinfo Tanzania, Edwin Urasa amesema wameona wazindue kampeni ya uchangishaji fedha itakayolenga watoto wenye mtindio wa ubongo walio chini ya miaka mitano.

“Kwa mwaka 2024 imewekwa lengo la kusaidia watoto 300 wenye mtindio wa ubongo nchini kwa kuwapa huduma ya kina ikiwa ni pamoja na ushauri, dawa, tiba ya mwili, huduma za maabara na picha,” amesema Urasa.

Amesema malezi ya kila mwaka ya mtoto mmoja yanagharimu Sh2 milioni.

Kutokana na hilo, amesema wamelenga kukusanya Sh100 milioni kwa ajili ya matibabu ya watoto 30.

Urasa amesema fedha hizo hazitashughulikia matibabu pekee bali zitachangia pia asilimia 10 ya lengo la mwaka la CCBRT katika eneo hilo.

Amesema uamuzi wa kuchangisha fedha hizo unatokana na rekodi ya kutoa huduma ya kina hasa katika kushughulikia mahitaji ya watoto wenye ulemavu wa ubongo.

Urasa amewaomba Watanzania kuungana kuwasaidia watoto hao.

Mkurugenzi wa CCBRT, Brenda Msangi amesema wanahudumia watoto takribani 3,000 kwa awamu moja na kwa mwaka huhudumia watoto 9,000.

“Mchango utakaotolewa utatusaidia sisi na wazazi, kwani kuna mahitaji muhimu ambayo yanahitajika. Tunatoa huduma ya utengemao hususani kwa watoto wenye mtindio wa ubongo, na tunatakiwa kutoa matibabu endelevu,” amesema.

Related Posts