LICHA ya Simba kutajwa timu yenye mafanikio kwenye miaka ya hivi karibuni kutokana na rekodi nzuri kimataifa ikiwa namba tano kwa ubora Afrika ndio timu pekee ambayo imefundishwa na makocha tisa ndani ya misimu sita.
Simba imeandika rekodi hiyo ya kuachana na makocha hao baada ya juzi kuachana na Abdelhak Benchikha ambaye amedumu kwenye kikosi hicho kwa siku 157 pekee akiwa ndiye kocha aliyeshika nafasi ya pili kwa kukaa muda mfupi zaidi.
Ndani ya misimu sita Simba ilianza na Pierre Lechantre ambaye alijiunga na timu hiyo Januari 2018 na kuondoka Juni 2018, baada ya hapo Julai 2018 ilimpa mkataba Patrick Aussems ambaye pia hakudumu kikosini akaondoka Novemba 2019.
Desemba 2019, Sven Vandenbroeck alitua Simba akiiongoza timu hiyo kutwaa mataji mawili ingawa naye Januari 2021 alitimka kikosini na ndipo ikamnasa Didier Gomes Januari 2021 kisha akatimka Oktoba 2021.
Novemba 2021, Pablo Franco alitua kuinoa Simba alihudumu miezi sita ndani ya kikosi hicho baada ya Mei 2022 kutimka na nafasi yake kuchukuliwa na Zoran Maki Juni 22 na kuondoka Septemba 22 ikiwa ni kocha aliyedumu muda mfupi zaidi.
Septemba 2022, mzawa Juma Mgunda alipata nafasi ya kuifundisha Simba akihudumu kwa miezi mitano na kujiwekea rekodi ya kuiongoza timu hiyo kwenye mechi 18 kati ya hizo alifungwa moja tu, akaachana nayo Januari 2023.
Januari 2023 Simba ikamtangaza, Roberto Olivieira ‘Robertinho’ ambaye aliiongoza kwenye mechi 12, akishinda michezo saba, alifungwa mmoja dhidi ya watani wao Yanga mabao 5-1, ikawa ndio safari yake imeishia hapo.
Benchikha akiwa amedumu kwa siku 157 tangu alipoajiriwa Novemba 24 na kutambulishwa siku nne baadaye akichukua nafasi ya Robertinho, ameiongoza timu hiyo katika michezo 21 ya mashindano yote ikiwemo ya Ligi Kuu, Ligi ya Mabingwa Afrika, Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na Ligi ya Muungano iliyorejea mwaka huu.
Katika Ligi Kuu Bara ameiongoza katika michezo 11 ambapo kati ya hiyo ameshinda sita, sare tatu na kuchezea kichapo mara mbili huku akifunga jumla ya mabao 18 na kuruhusu nyavu za kikosi hicho kutikiswa mara nane tu hadi sasa msimu huu.
Ni michezo miwili tu ya Ligi Kuu Bara ambayo Benchikha hakuiongoza Simba ambayo ni dhidi ya Coastal Union ambayo timu hiyo ilishinda mabao 2-1 (Machi 9, 2024) na ushindi wa 3-1 mbele ya Singida Fountain Gate uliopigwa Machi 12, mwaka huu.
Mwanaspoti limezungumza na makocha waliowahi kuifundisha timu hiyo wamefunguka mambo mbalimbali na kuwakingia kifua makocha huku wakikiri shida ipo ndani ya uongozi.
MAKOCHA, MASTAA WAFUNGUKA TATIZO
Kocha na mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Abdallah ‘King’ Kibadeni alisema suala la kocha, Benchikha kuondoka lina mambo mengi nyuma yake licha ya sababu kuelezwa anakwenda kwao Algeria kwa ajili ya kutatua changamoto za kifamilia.
“Huenda angeenda na kurudi tena ila ameona CV (wasifu) wake unazidi kushuka jambo ambalo anaona ni bora kuondoka mapema, suala la matokeo pia ni changamoto kwa sababu kama timu haifanyi vizuri yeye ni mtu wa kwanza kulaumiwa,” alisema.
Kwa upande wa nyota wa zamani wa timu hiyo, Mtemi Ramadhan alisema, anaona shida kubwa iko kwa viongozi na wachezaji kwa sababu licha ya makocha wengi waliopita kuonekana bora ila bado changamoto kwao imekuwa kutodumu kwa muda mrefu.
“Mimi naweza kusema hata kama akija kocha mkubwa lakini ikiwa wachezaji hawajitumi ni kazi bure, Benchikha hakuna ambaye hajui uwezo wake, sasa ukiniambia ni kutokana na matatizo ya kifamilia pekee yaliyoanishwa sikubaliani nalo kabisa.”
Mtemi aliongeza, kuna muda unaona wachezaji hawajitumi kabisa yaani wanacheza michezo ya kimashindano kama mechi za kirafiki.
“Kuna makocha walikuja Simba na wakaondoka kwenye mazingira ya aina hii ila walikokwenda wanafanya vizuri, mimi naona shida iko labda kwa viongozi kwa sababu kama hawapati mahitaji yao kwa wakati ni lazima tu watacheza chini ya kiwango.”
Kocha wa Singida Fountain Gate ambaye amewahi kucheza Simba na kufundisha, Jamhuri Kihwelo alisema, tatizo la Simba ni la muda mrefu halijaanza hivi karibuni na makocha hawana shida yoyote.
“Nilisema wamuache Juma Mgunda kwani hali sio nzuri na yule ni kocha mwenye uzoefu na alishaanza kuweka mambo sawa, lakini wakamleta Robertinho ambaye naye ni kocha mzuri ila alikuja muda ambao sio sahihi.
“Timu ipo Uturuki kocha hayupo, anakuja kujiunga wiki moja ya mwisho, dirisha la usajili likifika makocha hawapewi nafasi ya kusajili jambo ambalo linaongeza matatizo zaidi kwani wanashindwa kufanya kazi na machaguo ya watu wengine.
“Benchikha alipoingia naye anakuta na wachezaji wanakwenda kucheza Afcon huku kuna michuano ya kimataifa ambayo walivuka tu na kuishia robo fainali kwa kupambana sana, baada ya hapo wanarudi kwenye ligi na kuanza kupoteza na mashujaa, hivyo hawakuwa na muda wa utulivu na kujipanga mpaka kocha anaondoka.
“Kabla hajaletwa kocha mwingine basi wasirudie makosa waliyoyafanya huko nyuma, sasa wajipange wajenge timu ili mafanikio yapatikane,” alisema Julio.
Kocha wa zamani wa timu hiyo, Patrick Aussems amefunguka na kusema tatizo la Simba ni lilelile. Aussems aliyeinoa Simba kuanzia Julai 2018 hadi Novemba 2019, amesema tatizo la Simba kutodumu na makocha ni viongozi kutokuwa waadilifu jambo ambalo alilisema wakati anaondoka.
“Kuna sababu nyingi za makocha kuondoka lakini kwa Simba nadhani kuna shida kwenye uongozi kutokuwa waadilifu ‘unprofessional’. Hilo sio tatizo la Simba tu bali Afrika nzima viongozi wanataka kuingilia majukumu ya benchi la ufundi wakitumia vyeo vyao,” alisema Aussems ambaye kwa sasa yupo nyumbani kwake nchini Ufaransa na kuongeza;
“Naogopa, nadhani tatizo hilo litachelewa kumalizika hususani kama viongozi hawatataka kubaki kwenye vyeo vyao na kutimiza majukumu yao bila kuingilia ya wengine.”
Kocha huyo aliyeipa Simba makombe mawili, Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho (FA), sambamba na kuifikisha timu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, alisema watu hususani vyombo vya habari vinapaswa kupaza sauti ili kukomesha jambo hilo Afrika.
“Nimekuwa Afrika kwa muda na hilo ni tatizo sugu, nadhani njia pekee ya kulikomesha ni watu kuzungumza na kulikaripia hususani nyie wana habari,” alisema kocha huyo aliyeondoka Simba na kuchapisha andiko kwenye mtandao wake wa kijamii wa Instagram lililosomeka ‘Simba ili ikue inapaswa kuepukana na viongozi wasio na maarifa na waongo.’
Tangu kuondoka kwa Aussems mwaka 2019, Simba imefundishwa na makocha saba tofauti, Sven Vandebroeck, Didier Gomes, Pablo Franco, Zoran Maki, Juma Mgunda, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ na Benchikha. Wakati Benchikha akiwa ameondoka Simba tayari, timu hiyo itakuwa chini ya Juma Mgunda na Selemani Matola wakianza na mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo utakaochezwa leo Jumanne kwenye Uwanja wa Majaliwa, Lindi.