Hatua ya Umoja wa Ulaya kuaendelea kupokea mtiririko wa gesi kutoka Moscow ni kwa ajili ya kupasha joto kaya na makampuni yake, jambo ambalo hata hivyo linaongeza pia mapato ya Urusi.
Uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine ulipoanza mnamo Februari 24 mwaka 2022, viongozi wa Umoja wa Ulaya walilazimika kuzingatia utegemezi wao wa muda mrefu kwa gesi na mafuta vya Urusi. Gesi ilikuwa tatizo kuu hasa ikizingatiwa kuwa mnamo mwaka 2021, asilimia 34 ya gesi iliyokuwa ikitumiwa katika umoja huo ilitoka Urusi.
Nchi za Ulaya ya Kati na Mashariki zilikuwa tegemezi mno. Wakati Umoja wa Ulaya ulipochukua hatua ya kupiga marufuku manunuzi ya nishati hiyo, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz alidhihirisha wazi upinzani wake na kusema kuwa gesi na mafuta vya kuendesha shughuli za umoja huo, kwa wakati huo haiwezi kupatikana kwa njia nyingine yoyote ispokuwa kutoka Urusi.
Soma pia: Maoni: Putin amepoteza vita vya gesi na Ujerumani
Rais wa Urusi Vladimir Putin aliitumia vyema fursa hii na mnamo mwaka 2022, Urusi ilipunguza kiwango cha gesi kuelekea Ulaya. Viongozi wa umoja wa Ulaya (EU) walihofia kukumbwa na uhaba wa nishati hiyo muhimu hasa wakati wa msimu wa baridi. Ilikuwa ni hofu tu kwa maana EU haikuwahi kuidhinisha vikwazo madhubuti dhidi ya gesi ya Urusi.
Benjamin Hilgenstock mtaalam wa masuala ya kiuchumi kutoka Shule ya Kyiv ameiambia DW kuwa hatua ya EU haikuwa vikwazo bali uamuzi wa hiari na wa busara wa nchi hizo ili tu kutanua washirika zaidi wa ugavi ili kutokabiliwa tena na vitisho vya Urusi.
Gesi iliyosindikwa ya LNG
Kulingana na takwimu iliyotolewa na Umoja wa Ulaya, sehemu ya gesi ilioagizwa na nchi wanachama wa EU kupitia bomba la gesi la Urusi ilishuka kutoka jumla ya asilimia 40 mwaka wa 2021 hadi kufikia karibu asilimia 8 mwaka wa 2023.
Hata hivyo, ikiwa itajumuishwa gesi iliyosindikwa maarufu kama (LNG), ambayo ni gesi miminika inayoweza kusafirishwa kwa meli, jumla ya gesi ya Urusi iliyowasilishwa ndani ya Umoja wa Ulaya ilifikia asilimia 15 mwaka jana.
Soma pia: Urusi imelifunga bomba la gesi inayoingia Ujerumani
Kilichoiwezesha EU kupunguza utegemezi wake kwa gesi ya Urusi ni uamuzi wa kuongeza uagizaji wa gesi ya LNG kutoka nchi kama vile Marekani na Qatar. Walakini, hatua hii pia imesababisha bila makusudio kuongezeka kwa kiwango kikubwa cha gesi ya bei nafuu ya LNG ya Urusi kuingia katika Umoja huo.
Kwa sasa, Urusi ni msambazaji wa pili wa gesi ya LNG katika umoja wa Ulaya, hii ikiwa ni kulingana na kampuni ya ukusanyaji data ya Kpler. Tani milioni 15.5 ziliuzwa barani Ulaya mnamo mwaka 2023, ikiwa ni sawa na asilimia 16 ya usambazaji jumla wa gesi ya LNG ndani ya EU. Hii ni ongezeko la asilimia 40 ikilinganishwa na kiasi cha LNG kilichouzwa na Urusi kwa EU mnamo mwaka 2021.
Mwaka 2023, kiasi cha uagizaji wa gesi ya LNG kutoka Urusi kilipungua kidogo ukilinganisha na mwaka 2022, lakini data za robo ya kwanza ya mwaka huu wa 2024 zinaonyesha kuwa uagizaji wa LNG kutoka Urusi kuelekea Ulaya umeongezeka tena hadi kufikia asilimia 5 kwa mwaka, huku mataifa ya Ufaransa, Uhispania na Ubelgiji yakiwa ndio waagizaji wakubwa zaidi. Nchi hizo tatu zilichangia kwa asilimia 87 ya jumla ya gesi ya LNG ambayo iliwasilishwa ndani ya Umoja wa Ulaya mnamo 2023.
Soma pia: Ulaya haitonunua gesi ya Urusi kwa sarafu ya taifa hilo
Ingawa gesi ya Urusi bado inatiririka kuelekea Ulaya, mchango wake katika kiwango jumla cha uagizaji wa gesi barani humo kimeshuka kwa kiasi kikubwa tangu mwaka 2021. Umoja wa Ulaya unalenga kuachana kabisa na gesi ya Urusi ifikapo mwaka 2027, lengo ambalo wataalam wanasema linatekelezeka.